Uundaji wa istilahi za lugha yoyote ni sehemu ya ukuzaji wa lugha hiyo. Kadri jamii zinavyoendelea kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia ndivyo zinavyohitaji lugha mwafaka itakayoelezea maendeleo hayo. Kuna njia mbalimbali zinazotumiwa kuunda istilahi.
Katika lugha ya Kiswahili, misingi minne imekuwa ikitumika:
(a) Kiswahili chenyewe
(b) Lugha za Kibantu
(c) Lugha nyingine za Kiafrika
(d) Lugha za kigeni.
Misingi hii imetumiwa kwa mafanikio mbalimbali. Kuna wale waliosisitiza kuwa kabla hatujakopa istilahi kutoka lugha nyingine tutafiti Kiswahili sanifu na lahaja zake. Baada ya hapo tuchunguze uwezekano wa istilahi hiyo kuwepo katika lugha za Kibantu. Lakini tatizo lililopo ni kuwa lahaja za Kiswahili na lugha za kihuku hazijafanyiwa utafiti wa kutosha ili zitoe mchango kamili katika uendelezaji wa istilahi za Kiswahili. Kwa hivyo, mchango wake unapwaya.
Ukopaji kutoka lugha za kigeni bado unaendelea, japo una matatizo. Kiswahili kimeweza kukopa istilahi kutoka Kiingereza, Kiarabu, Kireno, Kifaransa, Kiajemi na Kihindi. Lugha kopeshaji hizi ni nyingi mno na hutatiza uimarishaji wa istilahi. Isitoshe, bado hatuna taasisi zinazoweza kutoa mwelekezo wa mara moja na hali aghalabu istilahi huhitajika mara moja ili kufaulisha mawasiliano. Tatizo la usawazishaji wa istilahi halina ufumbuzi wa moja kwa moja kwa sababu asasi ni chache mno.
Tatizo lingine ni mfumko wa visawe vya kiistilahi. Dhana moja inaweza kupewa visawe anuwai kutegemea, kwa mfano, lugha kopeshaji iliyotumika.
Kwa hivyo, unakuta visawe vifuatavyo:
- irabu (Kiarabu); vokali (Kiingereza)
- televisheni (Kiingereza); runinga (rununut + maninga) rukono (rununu + mkono); simu tamba
- barua-e; baruapepe
- utandawazi; utandarithi
- ntaneti; mdahalishi, n.k.
Bado kuna kazi nyingi katika usawazishaji wa istilahi. Hata hivyo, kuna mapendekezo ambayo hufuatwa kimataifa katika uundaji wa istilahi. Lengo hasa ni kuunda istilahi zinazoeleweka kwa urahisi na wanasayansi wengi, licha ya kutumia lugha tofauti za kitaifa katika mawasiliano ya kitaaluma.
Baadhi ya misingi mahususi ni:
- Istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazoziwakilisha (au angalau zidokeze hali inayokusudiwa). Pia, ziwe angavu kwa watumiaji. Kanuni hii inatuhimiza kuchunguza mwambatano na unyambulishaji wa mizizi ya maneno.
- Tukitumia mbinu ya muungano na mwambatano wa maneno ni muhimu tuzingatie:
(a) Idadi ya maneno yanayounganishwa au kuambatanishwa yasizidi mawili.
(b) Visawe visitumiwe kutenga istilahi ambatani. Kwa mfano:
- vidhibitimwendo
- sokohuria.
(c) Istilahi ziwe na uwezo mkubwa wa kunyambuliwa ili kuzalisha
istilahi nyingine.
Kwa mfano:
- taifa
- taifisha
- utaifishaji
- utaifa, n.k.
(d) Istilahi ziwe toshelevu-ziakisi sifa na dhana zinazolengwa.
(e) Istilahi ziwe fupi na zinazoeleweka.
(f) Kila dhana yafaa iwakilishwe na istilahi moja tu. Mfumko wa visawe uepukwe.
Katika harakati ya uundaji wa istilahi za Kiswahili, wakuzaji wamewahi kutumia mbinu mbalimbali: Baadhi ya mbinu hizo ni:
1. Matumizi ya visawe: Neno la kigeni kuchukuliwa kama kisawe cha neno la Kiswahili ambalo lipo. Kwa mfano: koromeo.
2. Muungano wa maneno. Kwa mfano:
(a) mwana + sheria = mwanasheria
(b) kiini + macho = kiinimacho
(c) pima + joto = kipimajoto
(d) mwana + kamati = mwanakamati.
3. Mwambatano wa maneno. Kwa mfano:
- nusu kipenyo
- kima cha juu.
Katika istilahi hizi mna matumizi ya viunganishi.
4. Unyambulishaji: Takriban vitenzi vyote vya Kiswahili vinaweza kun yambuliwa kwa kuambishwa. Kwa mfano:
- mtenga: utengano, tenganisha
- ongeza: nyongeza.
5. Upanuzi wa maana za maneno: Hapa neno huongezewa maana maalum ya kiistilahi. Ili kulifanya istilahi sharti kuzingatia mantiki ya uhusiano kati ya maana ya kawaida na ya kiistilahi. Kwa mfano:
(a) Tanzia:
- habari ya kifo
- aina ya kazi ya fasihi ambapo mhusika mkuu hupatwa na masaibu makuu yasiyowezekana. Mara nyingi mhusika mkuu huishia kifo.
(b) Kilele:
- sehemu ya juu ya mlima au mti
- upeo wa kazi ya fasihi.
6. Kukopa kutoka lahaja za Kiswahili. Kwa mfano:
- kimondo – ushairi wa malumbano (Lamu)
- poza – tuliza (Kimvita).
7. Kukopa kutoka lugha nyingine za Kibantu. Kwa mfano:
- ngeli (Kihaya)
- bunge (Kinyamwezi).
8. Kukopa kutoka Kiarabu. Kwa mfano:
- sifuri = bure, tupu, bila chochote maudhui = mawazo, mambo muhimu
- muktadha = msingi, kwa kurejelea.
9. Kukopa kutoka Kiingereza. Kwa mfano: virusi = virus
- silabi = syllable
- desimali = decimal.
10. Ukopaji sisisi. Kwa mfano:
- ncha ya ulimi
- ala za matamshi
- mahala pa kutamkia
- bapa la ulimi.
Kwa hivyo kuna mbinu aina mbalimbali za kuunda istilahi za Kiswahili.