Wasifu ni maelezo kuhusu jinsi mtu, kitu au mahali panavyoonekana. Wasifu wa mtu, kwa mfano, unajumlisha sifa za maisha yake, maumbile na pengine tabia zake. Mara nyingi, sifa zinazosisitizwa ni mchango wa mtu katika tukio la kijamii kama vile siasa, uchumi, usomi, n.k. Mwenendo wa matusi au kashfa haukubaliki katika tungo za kubuni zinazokusudiwa kuwaelimisha wanadamu.
Ufuatao ni wasifu wa mwasisi wa umoja wa watu weusi barani Afrika, marehemu Kwame Nkrumah.
Mfano wa wasifu
WASIFU WA KWAME NKRUMAH
Kwame Nkrumah alizaliwa mwaka wa 1909 mashariki mwa nchi ya Ghana. Alipata masomo yake katika Chuo cha Achimota nchini Ghana, Marekani na pia Uingereza.
Alijingiza katika siasa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Alikuwa katibu wa chama cha UGCC. Katika mwaka wa 1949, alianzisha chama chake cha CPP.
Baada ya uchaguzi wa mwaka wa 1954, Nkrumah aliibuka mshindi na kuwa waziri mkuu. Ghana ilipokuwa Jamhuri mwaka wa 1960, Nkrumah alikuwa Rais wa kwanza.
Nkrumah alikuwa na ari kuu ya kupigania hali ya Waafrika. Aliunga mkono wapiganaji wa ukombozi katika nchi zingine bila uoga. Isitoshe, aliwaunga mkono viongozi wa Kiarabu kama vile Abdel Nasser walipokuwa wakijaribu kujinasua kutoka kwa minyororo ya kikoloni na ukoloni mamboleo. Nkrumah alistahi uafrika wake zaidi kuliko uraia wake.
Kwame Nkrumah alikuwa miongoni mwa viongozi waliopinga ubaguzi wa rangi katika nchi ya Afrika Kusini. Aliona hali hiyo kuwa udhalimu wa kiwango cha juu.
Rais Kwame Nkrumah alitaka sana kuyaboresha maisha ya watu wa Ghana. Ili afaulu katika kulitekeleza hili, alihitaji kiasi kikubwa cha pesa. Katika miaka yake ya kwanza kama kiongozi, mmea wa kakao ulikuwa ukiiletea nchi hiyo pesa nyingi sana. Kwa hivyo, nchi ya Ghana ilikuwa na pesa za kutosha za kakao kuendeleza miradi mbalimbali. Baada ya mwaka wa 1963 bei ilishuka sana. Ilimbidi Nkrumah kulipia miradi aliyokuwa ameshaanza na huku pesa za matumizi zikiadimika. Hata hivyo, alifanikiwa kujenga mtambo mkubwa wa kusambaza nguvu za umeme uitwao Bwawa la Volta (Volta Dam).
Ingawa alijaribu sana kuiendeleza sana nchi yake, kuna wale waliomwon kama mtu dhalimu. Mambo yalimharibikia zaidi Ghana ilipojikuta na maden mengi.
Mwaka wa 1966, Nkrumah alifanyiwa mapinduzi ya kijeshi alipokuwa safarini. Nkrumah alienda uhamishoni katika nchi ya Guinea. Aliaga dunia akiwa katika nchi ya Romania mwaka wa 1972 akiwa anapewa matibabu.
Alifanyiwa mazishi ya kitaifa. Anakumbukwa kama kiongozi shupavu katika harakati za uhuru wa nchi ya Ghana na mwasisi wa Umoja wa Watu Weusi.
Zingatia: Mambo muhimu yanayosimuliwa katika maisha ya Nkrumah ni:
(i) kuzaliwa kwa Nkrumah.
(ii) mchango wake katika ukombozi wa nchi ya Ghana na Bara la Afrika.
(iii) matatizo ya kiuchumi yaliyosababisha kuporomoka kwa Serikali yake.
(iv) kifo chake.