Baruameme ni barua inayopelekwa kupitia mdahalishi (intaneti). Barua hii inaweza kuwa na viambatanishi kama vile picha, makala, video na sauti. Faili hii inayoambatanishwa hukodewa katika taratibu za ukodaji kama vile MIME. Mpokeaji wa baruameme sharti aikodae hiyo barua kwa kutumia utaratibu wa kukoda uliotumiwa. Akishaikodua, ataisoma kama ilivyotumwa bila ya mabadiliko yoyote.
Ukipeleka baruameme kwa njia ya mdahalishi, barua hiyo hupitia viunganishi kadhaa kabla ya kufikia mpokeaji.
Orodha ya barua huwaungamanisha watu wenye maslahi sawa, kwa mfano, wachora vibonzo wa Afrika Mashariki. Mmoja wa washiriki akipeleka barua hiyo kwa wenye orodha ya barua, huwasilishiwa kila mmoja wao. Ili jina lako liongezwe kwenye orodha ya barua unatakiwa kumwandikia msimamizi wa orodha hiyo na umpe jina lako.
Pamoja na anwani yake ya baruameme, ikiwa mtu anataka kujiunga na orodha ya baruameme mtu huyu huandikia kompyuta barua badala ya kuandikia mtu binafsi. Kompyuta hiyo iitwayo “mhudumu orodha” itasoma barua hiyo na kuingiza jina lako kwenye orodha. Unaweza kujiondoa kwenye orodha kwa njia hiyo hiyo.
Utaratibu wa Baruameme:
- Andika barua. Ukitaka kuambatanisha picha, programu, sauti, video na daftari zingine fanya hivyo kwa kuelekeza kielekezi kwenye kisanduku cha “Ambatishana”. Fuata maelekezo ya kompyuta unapoambatanisha na ubofye visanduku vinavyofaa.
- Penye mstari wa “kwa” piga chapa anwani ya mpokeaji. Zingatia kila alama katika kupiga chapa anwani. Ukikosea herufi au kistari, barua itadunda na haitamfikia mlengwa wako.
Kwa: belyons@africaonline.co.ke
Kutoka kwa: oldiasis@nbinet.co.ke
Mada: Harusi ya Achieng’
- Penye mstari wa mada, piga chapa mada ya ujumbe wako au muhtasari mfupi sana. Kwa mfano:
Harambee Stars yailaza Simba Stars njoo tusameheane
- Andika ujumbe wako kwa kifupi.
Kwa mfano:
Said:
Hivi majuzi nilikuwa Mombasa. Nilishangazwa na ufundi wa timu ya Harambee Stars. Saidi hebu nieleze: Unafahamu mfadhili wa Harambee Stars? Nataka kumwandikia barua nimhongere kwa msaada aliotoa kwa Harambee Stars. Asante.
Nduguyo J. Maadili
- Andika jina lako na ueleze kielezi kwenye kisanduku kilichoandikwa “Tumia”.
- Barua yako itapelekwa kama pakiti kupitia utaratibu wa TLP/IP mdahalishi (intaneti). Kila pakiti ina anwani ya mpokeaji.
- Pakiti zikishafika kwenye anwani ya upokezi huunganishwa na kufanywa ujumbe utakaosomwa na mpokeaji.
- Unaweza kuwapelekea watu mbalimbali barua yako. Ukitaka kutalii wavuti za Kiswahili, ingia mdahalishi kupitia: http://www.google.com/intl/sw/