SARUFI – VIWAKILISHI: VIONYESHI, VIMILIKISHI, VIULIZI, VIREJESHI, A-UNGANIFU

Viwakilishi ni aina ya maneno katika sarufi ya lugha yenye uamilifu wa kusimamia nomino kwenye miktadha mbalimbali.

(a) Viwakilishi vionyeshi

Viwakilishi hivi vinaonyesha (vinaashiria). Hujengwa na mzizi pamoja na kiambishi cha upatanisho wa kisarufi wa nomino inayohusika. Umbo la mzizi hutegemea umbali au ukaribu wa uonyeshi. Kwa mfano, mzizi -le hutumiwa kuonyesha umbali na konsonanti h na irabu huonyesha ukaribu. Tazama mifano ifuatayo, huku ukizingatia kuwa vionyeshi hivi vinategemea ngeli.

  • Nomino zilizo karibu kabisa na msemaji:

huu, hizi, hapa, hili, haya, huku, hiki, hivi, humu

  • Nomino zilizo mbali kidogo na msemaji:

hao, huyo, huo, hiyo, hilo, hayo, hicho, hivyo, hii, hizo

  • Viwakilishi vionyeshi vya mbali

Mzizi utumikao katika viwakilishi hivi ni -le. Viambishi vya upatanisho wa kisarufi wa nomino inayohusika na vionyeshi hutokea kabla ya mzizi wa uonyeshi.

Kwa mfano:

UmojaWingi
yulewale
ulezile
ilezile
lileyale
kilevile
ulezile
kuleØ
paleØ
mleØ

(b) Viwakilishi vimilikishi

Viwakilishi hivi vinahusishwa na dhana ya umiliki. Pia umiliki unahusishwa na nomino kwa sababu ndizo zinazomiliki. Ili kuunda viwakilishi vimilikishi mizizi ya viwakilishi huungana na viambishi vya upatanisho wa kisarufi kutegemea nomino inayohusika na umiliki. Mizizi hiyo ni:

UmojaWingi
-angu-etu
-ako-enu
-ake-ao

(c) Viwakilishi viulizi

Hivi vina uamilifu wa kuuliza maswali yanayorejelea nomino. Tunaweza kuvigawa katika makundi matatu:

(i) Vya mzizi – pi:

Kwa mfano:

UmojaWingi
yupiwapi
upizipi
ipizipi
lipiyapi
kipivipi
upiipi
kupiØ
papiØ
mpiØ

Zingatia kwamba mzizi -pi unatanguliwa na kiambishi cha upatanisho wa kisarufi wa nomino inayohusika.

(ii) Vya mzizi -nga- na- – pi:

Katika kikundi hiki -nga- inaonyesha dhana ya idadi na -pi dhana ya kuuliza.

Kwa mfano:

  • ngapi
  • wangapi
  • mingapi
  • mangapi
  • vingapi
  • pangapi.

Viwakilishi hivi vinahusu nomino za wingi tu. Ni viwakilishi viulizi vya idadi.

(iii) Vya mzizi -ni:

Hivi vinahusu:

(i) mtu anayehusika na kile kisemwacho.

(ii) jambo linalohusika na kile kisemwacho.

(iii) muda unaohusika na kile kisemwacho. Kwa mfano:

nani, nini, lini, gani.

(d) Viwakilishi virejeshi

Hivi hurejelea nomino inayosimamiwa. Huundwa kwa amba-, kiambishi cha upatanisho wa kisarufi wa nomino inayosimamiwa, na kiambishi cha O-rejeshi. Katika ngeli ya kwanza, mzizi amba- unaandamana na kiambishi -ye peke yake. Tazama mifano ifuatayo.

UmojaWingi
ambayeambao
ambaoambayo
ambayoambazo
ambachoambavyo
ambaloambayo
ambako
ambapo 
ambamo

(e) Viwakilishi vya A-unganifu

Viwakilishi hivi hutegemea nomino na huunganisha nomino na sehemu zingine za sentensi. Huongozwa na ngeli ya nomino inayohusika. Tazama mifano ifuatayo:

  • Mtoto wa shule
  • Kitabu cha mwanafunzi
  • Mahali pa starehe
  • Maji ya kunywa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *