SARUFI -MUUNDO WA SENTENSI: SHAMIRISHO (KIPOZI, KITONDO, ALA/KITUMIZI) NA CHAGIZO

Tazama sentensi hii:

Kato                                    alimpeleka mfungwa jana

(Kundi Nomino)                  (Kundi Tenzi)

Ugawaji wa sentensi katika mafungu hayo mawili ya KN na KT ulitanguliwa na utaratibu wa kugawa sentensi katika vikundi vya kiima na kiarifu. Katika utaratibu huo kiarifu cha sentensi hiyo hapo juu ni “alimpeleka mfungwa jana”. Kiarifu hicho kinaweza kugawanywa katika kitenzi, shamirisho na chagizo.

Shamirisho ni sehemu ya kiarifu inayotokea baada ya kitenzi kikuu; na chagizo ni sehemu inayokuja baada ya shamirisho, hasa ikiwa inafafanua kuhusu kitenzi. Kwa hivyo:

Kiima:                    Kato

Kitenzi:                 alimpeleka

Shamirisho:        mfungwa

Chagizo:               jana

KIIMAKITENZISHAMIRISHOCHAGIZO
Odarialikulachakulavizuri
LenaalichezavoliboliKwa bidii
Wazirialifunguahospitaliya kifua kikuu

Chagizo ni nafasi vinamokaa vielezi kwenye sentensi na kwa kawaida huja baada ya kitenzi ijapokuwa huweza kusimama mahali popote katika tungo.

Vielezi vya aina yote; vya namna (jinsi), vya idadi, vya mahali na vya wakati huweza kuunda chagizo.

Neno shamirisho hutumiwa kusimamia vitendwa na vitendewa vinapotokea katika Kundi-Tenzi (KT). Nomino hii ya pili (KN2) hutawaliwa na KT ambapo KN, hutawaliwa moja kwa moja na S (Sentensi). Kwa mfano:

Msichana huyu alishinda wanafunzi ishirini.

                                                                        s
KN1                                               KT
N    V      T                               KN2
       N   E
Msichanahuyualishindawanafunziishirini

Zingatia:

  • shamirisho (wanafunzi)
  • chagizo (ishirini)

Ni muhimu kutambua kwamba kiambishi cha kitendwa/kitendewa pia ni

shamirisho. Kwa mfano:

  • Mwanafunzi ananipenda.
  • Wanafunzi wanatuheshimu.

KIPOZI NA KITONDO

Sentensi zinaweza kupambanuliwa kwa msingi wa maana. Ili kufanya hivyo, tunachunguza dori za maana (namna nomino mbalimbali zinavyotekeleza majukumu katika sentensi). Kila kitenzi hutoa taarifa kuhusu nomino. Nomino yaweza kuwa mtenda (mtu au kitu kinachofanya jambo) na kiima hicho ni kiima halisi. Nomino pia yaweza kuwa mtendwa (kipozi), au mtendewa (kitondo).

Kwa hivyo basi, kipozi ni jina la kitu au mtu anayepokea pigo au uzito unaoashiriwa na kitenzi na kuubeba. Kipozi ni kitu kinachopoza tendo; kinachofikiwa na tendo moja kwa moja. Kitondo ni jina la kitu au mtu wa tatu anayefanyiwa jambo. Mtu au kitu cha kwanza hutenda (ni mtenda); uzito au nguvu za tendo hilo hufikia kipozi; kupitia kipozi, kitondo hufikiwa na tokeo la hicho kitendo kwa hasara au faida. Nomino hii ya tatu inaitwa kitondo kutokana na neno mtondo (yaani siku baada ya keshokutwa; siku kabla ya mtondogoo). Kitondo ni kama mfadhiliwa; anayefanyiwa jambo. Kitenzi huelekeza kama nomino ni kitenda; mtendwa (kipozi) apokeaye uzito wa kitenzi; au mtendewa (kitondo).

Katika tungo yakinishi na kanushi, kipozi na kitondo ni sehemu ya shamirisho. Tazama mifano hii hapa:

• Wanafunzi wanapika ugali.

mtenda: wanafunzi

kipozi: ugali (mtendwa)

• Mama alimpikia mtoto uji.

mtenda: mama

kipozi: uji

kitondo: mtoto (mtendewa)

M

Katika tungo yakinishi na kanushi za kauli ya kutendewa, kipozi na kitondo huwa kiima cha tungo. Kwa mfano;

• Ugali ulipikwa na mama.

• Mtoto alipikiwa uji na mama.

SHAMIRISHO ALA/KITUMIZI

Tumeona kwamba tunaweza kuwa na:

• Shamirisho kipozi: Baba anajenga ukuta.

• Shamirisho kitondo: Baba anamjengea mkwewe ukuta.

Mkwewe: kitondo

ukuta: kipozi

Shamirisho ala ni Kundi Nomino inayoonyesha kifaa au chombo kilichotumiwa kutendea jambo, kama vile kalamu, nyundo, jembe. Kwa mfano:

(i) Mgonjwa alisafiri kwa gari.

(ii) Mwanafunzi aliandika kwa tarakilishi.

Kwa sababu sentensi hizi zina Kihusishi (H) kwa pamoja na nomino, zina shamirisho: ala (kitumizi). Kundi Nomino (KN) ina Shamirisho ala inayoashiria kwa kihusishi pamoja na nomino. Lakini inawezekana pia kutumia viambishi tamati: -ia, -lia (katika sentensi yakinishi au -lii au -ii (katika sentensi kanushi) ili kubainisha chombo kilichotumika. Kwa mfano:

(i) Aliandikia penseli.

(ii) Haandikii tarakilishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *