FASIHI: NGOMEZI

Ngomezi ni aina ya fasihi simulizi inayoshughulisha ngoma. Kwa karne nyingi, jamii za Kiafrika zilitumia ngoma kupitishia ujumbe fulani mahsusi. Ngoma hizo zilisemekana kuwa “zinazungumza”, yaani zinawasiliana na hadhira au wanajamii. Aina hii ya mawasiliano ingalipo katika jamii mbalimbali. Aidha, ngomezi ni “fasihi ya ala” za mahadhi. Ala za mahadhi ni ala za muziki zinazotoa sauti kama usemi wa binadamu. Kuna ala za jadi zilizotumika barani Afrika kama ala za mahadhi. Ala hizi ni baragumu, zumari, na ngoma. Baragumu (siwa) huwa na vishimo viwili vya kupelekea habari. Mpigaji hutumia dole kuzuia au kuruhusu hewa inayowezesha kuwepo kwa lugha ya ishara. Zumari pia ina vishimo vya kupimia hewa ili maana itakikanayo itokeze.

Lakini ala ya mahadhi iliyoimarika zaidi ni ngoma. Ngoma zinazotoa ujumbe zinapatikana miongoni mwa Waigbo na Waibibio wa Nigeria; Walokele wa Zaire, Akan wa Ghana na Wayoruba wa Nigeria. Umaarufu wa ngoma umeufanya usanii huu kuitwa ngomezi. Msanii hupitia mafunzo ya miaka mingi ili aweze kutunga ngomezi. Ngomezi hupatikana zaidi katika jamii zinazozungumza lugha ya kiimbo. Lengo ni kupiga ngoma kwa mdundo wa kiimbo cha usemi utakikanao hivi kwamba msikilizaji anahisi kama anamsikiliza mtu akiongea. Msanii hujitahidi ili maneno ya ngoma yake yasilete utata. Kwa hivyo, msanii anatumia mtindo wa “paukwa – pakawa” na takriri nyingi. Urudifu huu (kurudiarudia) wa semi humwezesha mlengwa kufahamu kinachoendelea.

Sifa za za Ngomezi

Ngomezi ni msimbo wa mawasiliano unaojulikana au kutambuliwa na maeneo fulani mahsusi ya watu au kabila. Maana ya mipigo ya ngoma, kwa mfano, hutambuliwa na jamii inayohusika tu. Ni vigumu kwa wageni kutambua maana ya midundo hiyo.

Ngomezi ni lugha ya mahadhi pasina maneno. Wanajamii wenyewe ndio ‘huvisha’ ngomezi maneno na maana tambuzi.

Usanii wa kupiga ngoma hutengewa kundi fulani mahsusi ambalo, mara nyingi, hurithishana kivizazi.

Ngomezi huchezwa mahali pamoja maalum kama vile:

(i) vilingeni panapopungwa mapepo.

(ii) sebuleni au jukwaani penye tafrija.

(iii) kumbini penye jando na unyago, n.k.

Umuhimu wa Ngomezi

Ngomezi hutumiwa katika kutekeleza kazi zifuatazo:

(i) kuita watu kujumuika.

(ii) kuwaburudisha watu.

(iii) kuwatibu watu kiganga.

(iv) kuwatanabahisha watu kuhusu hatari (kutoa ujumbe).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *