Vitendawili ni kauli za mafumbo. Kauli hizi ni fupi na zina maelezo ya kuteka akili ya msikilizaji kwa lengo la kudai ufumbuzi au uteguzi. Vitendawili hutumia lugha fasaha, aghalabu yenye miigo ya sauti au mapigo (tanakali za sauti). Aidha, hutumia lugha ya picha.
Tazama mifano ifuatayo:
(i) Nzi hatui juu ya damu ya sima (taswira inayopatikana ni MOTO. Hakuna “kinachotua” juu ya moto isipokuwa maji).
(ii) Chukua nikuchukue (tanakali za sauti. Jawabu ni KIATU). (iii) Huko ‘ng’o’ na kule ‘ng’o’ (tanakali za sauti. Jawabu ni GIZA). (iv) Parrrrr…. hadi Makka (mwigo wa sauti. Jawabu ni UTELEZI).
Umuhimu wa vitendawili
Vitendawili vina majukumu yafuatayo ya kijamii:
Kunoa bongo: Afumbiwaye fumbo la kitendawili hulazimika kutumia maarifa yake kulifumbua. Kufikiri kwa kina humwimarisha mtu kiakili.
Kuelimisha jamii: Kwa vile mazingira ya vitendawili yanategemea tajriba zetu, watoto na hata watu wazima huelimishwa navyo.
Kuchangamsha: Jamii nyingi enzi za kisogoni zilijitumbuiza kwa kutegeana vitendawili. Nafasi hii sasa inachukuliwa na vitumeme nyakati zetu.
Kukuza utamaduni: Vitendawili hutaja mazingira mbalimbali ya wanajamii husika na hivyo kukuza na kuendeleza utamaduni huo. Kwa mfano, jamii zinazokuza minazi zina vitendawili vinavyofafanua utamaduni huo wa minazi.
Tanzu za Lugha: Kidato cha Tatu
Kwa mfano:
(i)
A: Kitendawili.
B: Tega.
A: Di haina mshindo.
B: Jawabu ni DIFU.
(ii)
A: Kitendawili.
B: Tega.
A: Mwenye kuitwa amefika lakini mjumbe bado hajarudi.
B: Jawabu ni NAZI NA MKWEZI.