(a) Vitenzi vya kigeni
Katika Sarufi ya Kiswahili, kuna vitenzi vya kigeni ambavyo hutumiwa katika uundaji wa nomino. Kwa mfano:
Kitenzi cha Kigeni | Nomino Inayovyazwa |
Fahamu | Ufahamu |
Safiri | Safari, Msafiri, Usafiri |
Sahau | Usahaulivu |
Samehe | Usamehevu, Msamaha, Msamehevu |
Afiki | (Ma)afikiano |
Ahidi | Ahadi |
(b) Vitenzi vya kuambisha viambishi
Nomino mbalimbali huundwa kwa kuambisha viambishi katika vitenzi kama ilivyo hapa chini:
(a) Kiambishi awali ‘m‘
Kiambishi hiki huambishwa ili kuonyesha mtendaji
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
Safiri | Msafiri |
Hakiki | Mhakiki |
Rithi | Mrithi |
Zuka | Mzushi |
Sajili | Msajili |
(b) Kiambishi tamati ‘o’
Kiambishi hiki huambishwa kuonyesha tokeo la kitendo.
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
Jaribu | Jaribio |
Tisha | Tisho |
Funza | Funzo |
Lenga | Lengo |
Nena | Neno |
(c) Kiambishi awali ‘ki’
Kiambishi hiki kinapoambishwa huonyesha kitu kilichotumika
kufanyia tendo.
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
ziba | kizibo |
chunga | kichungio |
bana | kibanio |
(d) Kiambishi tamati ‘ji’
Kiambishi hiki kinapoambishwa huonyesha hali ya mazoea ya mtendaji.
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
Chora | Mchoraji |
Saka | Msakaji |
Fuga | Mfugaji |
(e) Kiambishi awali ‘ku’
Kiambishi hiki huambishwa ili kuonyesha kitenzi-jina kutokana na
kitenzi hicho.
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
Fadhili | Kufadhili |
Ghilibu | Kughilibu |
Soma | Kusoma |
(f) Kiambishi ‘u’ awali
Kiambishi hiki huambishwa ili kuonyesha udhahania.
Udhahania ni kinyume na uhalisi; ni fikra, hali ya kufikiria jambo lisilogusika wala kuonekana.
Mifano:
Kitenzi | Nomino |
Ogopa | Uoga |
Tafiti | Utafiti |
Teua | Uteuzi |
Funza | Ufunzaji |
Choka | Uchovu |
(g) Kiambishi tamati ‘i’
Kiambishi hiki kikiambishwa kwenye kitenzi huonyesha mtendaji na udhahania.
Mifano:
Kitenzi | Mtendaji | Udhahania |
Lea | Mlezi | Ulezi |
Asi | Mwasi | Uasi |
Pika | Mpishi | Upishi |
Kama inavyodhihirika hapo juu, inawezekana kuunda nomino kutokana na vitenzi. Nomino zilizoundwa huwa na maana maalum kutegemea kiambishi kilichoambishwa.