Katika upishi wa kisasa na wa kitaalamu, kuna maagizo au maelezo fulani mahsusi yanayoambishwa mapishi. Maagizo na maelezo haya hujulikana kitaalamu kama resipe.
Aidha, maelezo haya ni ya kisayansi, mepesi na yaliyokamilika kiasi cha kutumiwa na mtu yeyote anayepika chakula hicho. Taaluma ya resipe ina umuhimu wa pekee katika jumuiya za kisasa kwa vile inachangia katika uimarishaji wa utalii kupitia upishi bora hotelini.
Mfano wa resipe
Ufuatao ni mfano wa upishi bora wa kitoweo cha nyama.
KUPIKA NYAMA
Idadi ya walaji : 4
Viambato
- Nyama – kilo mbili
- Vitunguu – viazi viwili
- Mafuta – gramu hamsini
- Bizari – vijiko vya chai viwili
- Chumvi – kiasi
- Maji ya limau/tui la nazi – kikombe kimoja
- Iliki – mbili
- Dania – fungu moja
- Karafuu na mdalasini – kiasi
- Nyanya nne
Vifaa
- Sufuria safi
- Jiko la makaa, gesi au umeme
- Kijiko
- Maji safi
Hatua za kupika
- Safisha nyama vizuri kwa maji ya mfereji.
- Katakata nyama vipandevipande na kuiweka kwenye sufuria au kifaa kilichosafishwa.
- Safisha vitunguu, iliki, dania na nyanya kwa maji ya mfereji.
- Katakata viungo hivi na kuviweka kwenye sahani zilizosafishwa.
- Andaa jiko la makaa, gesi au umeme.
- Yeyusha/chemsha mafuta kwenye sufuria safi na uanze upishi wako.
- Mafuta yakishatokota, weka vitunguu, kisha ongeza nyanya vichemke hadi vitunguu vipate rangi ya zari.
- Ongeza bizari, chumvi, iliki, dania, karafuu na mdalasini.
- Viungo hivi vikiwa tayari, tia nyama kikaangoni na kuiacha kwa muda fulani ili iive.
- Ongeza maji kiasi ili kuandaa mchuzi mzuri.
Maandalizi
Nyama yaweza kupakuliwa kama kitoweo cha vyakula mbalimbali kama vile wali, ugali, githeri, chapati na vingine vingi.