AINA ZA MAANDISHI
Kuna aina tatu kuu za maandishi: nathari (tutumbi), tamthilia (natiki) na ushairi.
Nathari ni maandishi ya mfululizo na ya mjazo. Aidha, hupigwa mafungu ya sentensi, aya na sura au milango. Nathari hutoa maelezo marefu kuhusu kinachozungumziwa na mara nyingi huambisha mandhari maalum yanayomwezesha msomaji kujenga taswira fulani.
Tamthilia ni maandishi yaliyopangwa kimazungumzo ambapo watu au wahusika hupewa majina na maneno mahsusi ya kusema. Mazungumzo haya ni majibizano ambayo huenda sambamba na vitendo vya wahusika wenyewe. Licha kwa kina. Wahusika wanajengewa migogoro katika vitushi mbalimbali ambavyo ya kutaja vitendo vya wahusika katika mabano, mapambo ya mandhari huelezwa vimelenga maudhui fulani mahsusi.
Ushairi ni utungo wenye kunga ya maneno yaliyoteuliwa kwa ustadi mkubwa. Aidha, maneno ya kishairi hutumiwa kiistiara au kimafumbo. Maneno yenyewe yamepigwa mafungu ya mishororo na beti na mpangilio wake hutegemea ustadi wa mtunzi mwenyewe.
Uandishi wa Insha
Insha ni mtungo wa maneno yaliyoandikwa kwa mtindo wa nathari (tutumbi) au tamthilia (natiki) juu ya jambo mahsusi. Kwa ajili ya mitihani, utanzu wa ushairi haupewi sifa ya insha kwa vile ni maandishi teule.
Baadhi ya sifa muhimu za insha bora ni:
(i) matumizi ya lugha fasaha inayovutia kimatumizi.
(ii) matumizi ya lugha yenye mantiki na muwala.
(iii) matumizi ya maelezo yenye mguso kwa hisia za msomaji, yaani, lugha inayosisimua.
(iv) matumizi ya lugha sanifu iliyojengeka kwa msingi wa sarufi nzuri na msamiati mwafaka.
(v) kuzingatia kaida (kanuni) za uandishi zinazokubalika kimatumizi.
Aina za Insha
Kuna aina mbili kuu za insha:
(i) Insha za kawaida.
(ii) Insha Maalum (za kipekee).
Insha za kawaida ni insha zinazozingatia mtindo wa kimapokeo wa utangulizi, maelezo na hitimisho. Insha hizi ni kama vile insha ya masimulizi, mjadala, methali, maelezo, kubuni na wasifu.
Insha maalum au za kipekee ni aina za maandishi ambayo, licha ya kueleza jambo kimantiki, huchukua umbo au mtindo fulani mahsusi. Mtindo huu maalum ni kaida ya uandishi iliyokubaliwa kisifabia (kila mahali).
Insha hizo maalum zimetokana na mahitaji maalum ya kijamii kama vile mawasiliano ya kipekee, na kadhalika.
Mifano ya insha hizo maalum ni:
- ripoti maalum na ripoti ya kawaida
- kumbukumbu za mikutano
- hotuba
- barua rasmi na ya kirafiki
- mialiko
- resipe
- ratiba
- mazungumzo
- mahojiano
- dayalojia
- matangazo, n.k.