Katika utunzi wa kisanaa, kuna kitengo kinachohusiana na utoaji sifa za mtu au watu. Sifa za mtu zinaweza kutolewa na mtu mwenyewe (yaani, mwandishi) au na mtu mwingine.
Mara nyingi, sifa hizi hutolewa kutokana na matendo bora yenye utu yaliyotendwa na mhusika anayesifiwa. Tawasifu na wasifu huwa na kaida zinazokurubiana, japo kuna vipengee fulani vinavyozitofautisha.
(a) Tawasifu
- Tawasifu ni habari kuhusu maisha ya mtu zilizoandikwa na yeye mwenyewe. Yaani, mwandishi husimulia kisa chake.
- Masimulizi ya tawasifu, mara nyingi, huwa katika nafsi ya kwanza.
- Maandishi huchukua mtindo wa kiriwaya.
Mifano ya tawasifu:
- Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini, Shaaban Robert. Katika tawasifu hii, Marehemu Shaaban Robert anatueleza mambo mengi sana kuhusu maisha yake tangu utotoni, elimu yake, kazi mbalimbali alizofanya, ndoa zake na hata mauti ya mkewe wa kwanza.
- Miaka 52 Jela, P. Karanja. Mwandishi anatufafanulia madhila yake akiwa mfungwa.
Zingatia: Kwa vile tawasifu imeandikwa na mtu mahsusi kuhusu maisha yake mwenyewe, huenda huyo mwandishi akauficha ukweli fulani maishani mwake.
Aidha, anaweza kujipa sifa kupindukia au kusema uongo kuhusu tukio fulani maishani mwake. Mara nyingi, hakuna mtu apendaye kujikashifu au kutaja unyonge wake na mambo yanayomshushia hadhi.
MFANO WA TAWASIFU
UTANGULIZI WA TAWASIFU YA JOSHUA MPONDA
Nilizaliwa tarehe kumi na mbili mwezi wa saba mwaka wa Elfu moja mia tisa na thelathini na nne katika kijiji kidogo cha Masawa, eneo la Majujumili. Wazazi wangu walihamia Masawa kutoka Maputo. Kuumeni ni Mnyasa na kuukeni
Mshela.
Sikubahatika kulelewa na wazazi wangu. Inasemekana kuwa wote walikufa kutokana na mkurupuko wa ndui mnamo mwaka wa arobaini na moja. Mfadhili wangu, Bwana Krapf akanichukua hadi kambi ya Misheni Kuch ambapo aliniweka chini ya ulinzi wa Mama Mariamu, mlezi wa watoto yatima…
(b) Wasifu
- Wasifu ni kitabu au maandishi yanayoeleza maisha ya mtu mwingine. Yaani, mwandishi fulani mahsusi husimulia kuhusu maisha ya mtu mwingine.
- Maandishi ya kiwasifu hutumia nafsi ya tatu; pia huchukua mtindo wa kiriwaya.
- Inatarajiwa kwamba mwandishi wa wasifu atakuwa amefanya utafiti mwingi kuhusu maisha na kazi za yule anayeandika kumhusu.
- Tungo za wasifu hazina matusi au kashfa.
Mifano ya wasifu ni:
- Wasifu na Siti Binti Saad, Shaaban Robert.
- Maisha Ya Mohammed Hemed Said, Tippu Tipu.
- Mohamed Ali Chuma: Mwanasoka wa Tanzania, A. Mmallavi.
MFANO WA WASIFU
UTANGULIZI WA WASIFU WA SHAKILA BITISHOMARI
Bi. Shakila Bitishomari alizaliwa Mkunazili, Laini Moja huko Mkungulu mnamo 23/1/1956. Wazazi wake walikuwa Mwinyipembe Hassan na Mwajuma Pesamoja binti Yassin.
Alipata elimu yake ya msingi huko huko Mkunazili; shule ya upili akaenda Mwijiko kisha akasomea taaluma ya uhazigi, katika Chuo cha Leicester Medical College. Baadaye, alirudi nchini kuihudumia nchi yake ambapo umaarufu wake kama mkereketwa wa ukombozi wa nchi ulianza…