Tamathali ya usemi:SOGA

SOGA

Soga ni tamathali ya usemi ambayo ni kitumbuizo cha lugha. Aidha, huchukua mtindo wa mchezo wa kuigiza au hadithi fupi ambapo maneno yenye ulinganifu wa vina au sauti hutumiwa kimzahamzaha kwa lengo la kuchekesha.

Soga hutumiwa sana miongoni mwa watani au watu wa tabaka na umri mmoja kama njia moja ya burudani au starehe. Ifuatayo ni mifano ya matumizi ya soga.

Mifano ya soga

Mfano wa Kwanza

Raya: Rehema!

Rehema: (Akija mbio) Naam Raya, umeniita?

Raya: Sadakta, mbona unahema hivyo?

Rehema: Mimi sina hema kimwana. Nina nyumba ya msonge moja tu.

Raya: Hebu keti nikueleze mwenzangu (Rehema anaketi). Jana nimeota Kimaro.

Rehema: Ajabu kubwa. Mnyama gani huyo?

Raya: Acha mzaha Bwana. Humjui Kimaro?

Rehema: Lo! Kwani siku hizi ana joto la kutosha kuotwa? Ama ndio mwanzo kaota na kuchipuka?

Raya: Basi Rehema umeotea. Ninayosema ni kwamba nimemwona Kimaro usingizini.

Rehema: Na ulipomwona usingizini, alikuonya kuhusu oto la kuku wako, sio? (wanacheka).

Raya: Rehema, unaota ndoto gani hii ya kitoto?

Mfano wa Pili

Mchuuzi: (Akinadi sokoni) Haya, haya. Nyanya bei rahisi. Nyanya bei ya hasara.

Msafiri: (Akimkaribia) Ati nyanya bei rahisi. Una wazimu nini?

Mchuuzi: Bwana we, usiinyanyase biashara yangu bure bilashi.

Msafiri: Mimi sijapata kumsikia mtu akimuuza nyanyake sokoni. Ni ujuha uliokithiri. Huko ni kumnyanyasa nyanya. Isitoshe, nyanya ana thamani kubwa sana.

Amemzaa mamako ambaye atakuwa nyanyake mwanao kesho

Mchuuzi: Ee Bwana, siuoni mkoma wowote hapa. Vipi nitapata makoma yake? Itabidi uniombee kutoka kwa koma za mababu zetu.

Zingatia:

Maana ya pili ya soga ni mazungumzo ya kupitisha wakati au porojo za mtaani na vijijini. Aidha, porojo hizi hazina mashiko.

Tags: 33003300

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *