Viwakilishi ni aina ya maneno yanayosimamia nomino katika mikadha mbalimbali. Ijapokuwa viwakilishi husimania nomino, haina maana kwamba nomino inayowakilishwa huwa haipo kila mara. Kwa mfano, tusemapo “kitabu hiki”, hiki ni kiwakilishi cha nomino kitabu na maneno yote mawili yapo katika kifungu.
Kuna aina mbalimbali ya viwakilishi. Kwa mfano, viwakilishi nafsi, viwakilishi sifa, viwakilishi ngeli, viwakilishi pekee, viwakilishi idadi na vinginevyo.
(a) Viwakilishi sifa
Viwakilishi hivi husimamia nomino kwa kurejelea sifa za ‘kitu’ au ‘utu’. Kwa mfano:
(i) Tajiri aliwanyima wafanyakazi mshahara wao.
(ii) Mwizi amepora mali ya wahasiriwa.
(ii) Weusi wanadhulumiwa na weupe nchini Marekani.
(b) Viwakilishi nafsi
Haya ni maneno yanayosimama peke yake.
Viwakilishi nafsi ni kama vifuatavyo.
(i) Nafsi – huru
Umoja | Wingi | Nafsi |
Mimi | Sisi | Nafsi ya Kwanza |
Wewe | Ninyi | Nafsi ya Pili |
Yeye | Wao | Nafsi ya Tatu |
(ii) Nafsi tegemezi/viambata
Kwa hakika, hivi ni viambishi vinavyowakilisha nomino katika kujenga vitenzi.
Kwa mfano: ni-; u-; a-
- Nitakupeleka sokoni.
- Utanisaidia?
- Atatibiwa.
(c) Viwakilishi ngeli
Hivi ni viwakilishi vinavyoashiria ngeli ya nomino inayohusika. Ngeli zote zinaweza kuashiriwa. Kwa mfano:
- Kilipovunjika kilitupwa.
- Yalipopikwa yaliliwa na watoto.
- Yatachunwa kesho shambani.
(d) Viwakilishi vya Pekee
Hivi ni viambishi -enye; -enyewe; -ingine; -ote; -o-ote.
(i) enye: huonyesha umilikaji. Kwa mfano:
- Mwenye subira hulia kivulini.
- Mwenye pupa hali tamu.
- Mwenye gari amefika.
(ii) – enyewe: huonyesha msisitizo/mkazo. Kwa mfano:
- Alijitibu mwenyewe.
- Mgonjwa alijilaza kitandani mwenyewe.
(iii) – ingine: huonyesha zaidi ya; baadhi ya; sehemu ya. Kwa mfano:
- Watoto wengine huajiriwa viwandani.
- Vita vingine ni vya kikoloni.
- ·Mahali pengine pana usalama.
(iv) -ote: huonyesha kuhusika kwa wingi. Kwa mfano:
- Sheria zote zinawalinda watoto.
- Wasichana wote wamehitimu.
(v) -o-ote: huonyesha ‘kila’. Kwa mfano:
- Lolote laweza kunisaidia.
- Popote upendekezapo panafaa.
(e) Viwakilishi vya idadi
Hivi huonyesha idadi ya nomino. Idadi inaweza kuwa dhahiri au isiyo dhahiri kama ilivyo hapa chini:
(i) idadi dhahiri: wawili, wanne, ishirini, n.k.
(ii) idadi isiyo dhahiri: wachache, kadha, maelfu, n.k.
Kwa mfano:
- Wanafunzi wengi wamepita mtihani.
- Wakulima wachache wananufaishwa na mikopo.
- Maelfu ya watazamaji walishangilia mchezo wa soka.