Sentensi ya Kiswahili ina aina mbalimbali za maneno. Aina mojawapo ni kitenzi. Kitenzi ni aina ya neno linalotoa taarifa juu ya tendo lililofanyika au linalotendwa na kiumbe au kitu. Katika ufafanuzi wa vitenzi, tunaviainisha katika aina zifuatazo:
(a) vitenzi halisi
(b) vitenzi vikuu
(c) vitenzi visaidizi
(d) vitenzi vishirikishi vipungufu
(e) vitenzi vishirikishi vikamilifu
(f) vitenzi sambamba.
Je, unakumbuka aina hizi za vitenzi?
Aina za Vitenzi
(a) Vitenzi halisi
Kitenzi halisi kina nafasi kubwa katika sentensi ya Kiswahili. Hiki ndicho kitenzi kinachodhihirisha kuwa tendo limefanyika na huashiria muktadha wa kufanyika kwake. Ili kuashiria muktadha wa tendo, kitenzi halisi hujumlisha mambo yafuatayo:
- tendo lenyewe
- njeo/wakati na hali
- kauli ya kitenzi (kama kimenyambuliwa)
- hali ya kuyakinisha au kukanusha.
Kwa mfano:
Mgonjwa anatibiwa na daktari.
Kitendo halisi ni anatibiwa.
tendo – “tibu”
wakati – uliopo (‘na’)
kauli – tibiwa (‘tendewa’)
kuyakinisha – “ana”
(b) Vitenzi vikuu
Kitenzi kikuu ni kitenzi kinachoweza kujitokeza peke yake katika sentensi.
Kwa mfano:
Anapika.
Atamsaidia Cherop.
Musau atawatibu wagonjwa.
Mtoto alipelekwa shuleni.
Kitenzi kikuu ndicho kiini cha taarifa ya tendo na hakuna umbo lingine katika sentensi linaloarifu tendo. Vitenzi vikuu vina sifa nyingine: vina uwezo wa kufungamana na vipashio vingine katika sentensi. Yaani, huacha nafasi ili sentensi ijifafanue zaidi kupitia aina nyingine za maneno kama nomino na vivumishi. Kitenzi kikuu hujitokeza kama kitenzi halisi.
(c) Vitenzi visaidizi
Kitenzi kisaidizi ni kitenzi kinachoandamana na kitenzi kikuu.
Lengo ni kufafanua tendo au kulieleza zaidi.
Kwa mfano:
Nomino | Kitenzi kisaidizi | Kitenzi kikuu | Shamirisho |
Mgonjwa | aliyekuwa | anatibiwa | amepona. |
Mtoto | hakuwa | ameajiriwa | shambani. |
Sheria | itakuwa | ikifuatwa | na wananchi wote. |
Ali | alikuwa | akimpikia | dadake chakula. |
Katika sentensi zote hizo, ni dhahiri kuwa kitenzi kisaidizi kinatekeleza wajibu wa kufafanua kitenzi kikuu.
(d) Vitenzi vishirikishi vipungufu
Vitenzi vishirikishi huhusisha nomino au kiwakilishi chake kitabia, kihali au kimazingira.
Kwa mfano:
- Mwanakupona ni mkarimu.
Vitenzi vishirikishi vipungufu ni vile visivyoweza kuchukua viambishi vya wakati, ijapokuwa vinaweza kuchukua viambishi vya nafsi au majina ya ngeli. Viambishi vya vitenzi hivi ni kama vile ni-, si-, ndi-.
Kwa mfano:
- Auma ni hodari.
- Yeye ndiye mweka hazina.
- Lorupe si mnafiki.
- Sisi ndiswi wavuvi.
(e) Vitenzi vishirikishi vikamilifu
Vitenzi hivi ni vishirikishi vinavyochukua viambishi vya wakati.
Kwa mfano:
- Nanzala amekuwa mwerevu. (timilifu).
- Odari alikuwa baharini. (uliopita).
- Athman atakuwa nahodha. (ujao).
(f) Vitenzi sambamba
Vitenzi sambamba ni vile vinavyoambatana katika sentensi moja.
Kwa mfano:
Saida alikuwa hajawahi kwenda Unguja.
Katika sentensi hii alikuwa ni kitenzi kisaidizi na hajawahi kwenda ni kitenzi sambamba.