Kielezi ni neno linalotumiwa ili kuelezea zaidi juu ya kitenzi, kivumishi au kitenzi kingine. Mifano ya vielezi ni: sana, kabisa, mno, zaidi.
Sentensi:
- Mtoto amelala sana.
- Kitabu hiki ni kizuri mno.
- Kiongozi aliishiwa vibaya kabisa.
Zingatia kwamba maumbo ya vielezi hayaambikwi kwenye neno au katika upatanisho wake wa kisafuri. Lakini maumbo haya huweza kuradidiwa. Kwa mfano, unaweza kusema ‘sana sana’, ‘haraka haraka’, ‘pole pole’ na kadhalika.
Umbo la uradidi huwa linaelezea zaidi kuhusu kielezi kilichotangulia. Kwa mfano, ‘sana’, ya pili inafafanua kielezi ‘sana’ kilichotangulia.
Vielezi namna
Hivi hutumika kueleza namna kitendo kilivyotendeka. Kwa mfano:
- Alifanya kazi haraka.
- Alimweleza kinaganaga.
Vielezi namna ni vya aina hizi:
- vya halisi
- vya mfanano
- vikariri vya hali
- vya ala
- viigizi.
(a) Vielezi namna vya halisi
Haya ni maneno yanayotumika kama vielezi. Kwa mfano:
- Alicheza mpira barabara.
- Alishauriwa ajifunike kabisa.
(b) Vielezi namna vya mfanano
Hivi hujengwa kwa kuongezwa kiambishi ki (au vi) cha kupatanisha.
Kwa mfano:
- Diwani huyu anaongoza kikoloni.
- Mwendo wake si wa kike.
- Kufa kikondoo ndiko kufa kiungwana.
(c) Vielezi namna vikariri
Hivi hufafanua vitenzi kwa kurudia neno mara mbili.
- Anapenda kulala kifudifudi.
- Kikombe kilivunjika vipandevipande.
- Anakula kifisifisi.
- Alinyemelea kimyakimya.
(d) Vielezi namna vya hali
Hivi huonyesha vilitendeka kwa hali gani.
Waliwasili upesi.
Alisimama wima tangu asubuhi.
(e) Vielezi namna vya ala
Hivi hutaja chombo kilichotumika. Chombo chaweza kuwa cha uhisi, cha kugusa au cha kudhania.
- Alipigwa fimbo.
- Atadungwa sindano.
(f) Vielezi namna viigizi
Hivi hukariri na kuigiza mlio unaofikiriwa kutoka kitendo kitendekapo.
Kwa mfano:
- Amelala fofofo.
- Alifunga mlango ndi!
- Mbwa alibweka bwe!
Vielezi vya wakati
Hivi huonyesha wakati wa kitendo kutendeka. Kwa mfano:
- Alifika asubuhi.
- Tulikutana mwaka juzi.
- Tutakwenda Lamu mwakani.