Kielezi ni neno linalotumiwa kueleza zaidi juu ya kitenzi, kivumishi ama kitenzi kingine. Somo hili linashughulikia vielezi vya idadi, kiasi na mahali.
Soma kifungu kifuatacho ukizingatia maneno yaliyokolezwa wino.
“Mwakitele, ingia ndani unieleze jinsi mambo yalivyokuwa.”
“Sawa mzee. Mimi hukutii daima na sioni shida katika ombi lako.”
“Enhe. Karibu ukumbini. Eleza sasa.”
“Mzee, tulianza safari yetu juzi asubuhi. Kwa kipindi cha saa moja, dereva wetu alionekana mchangamfu kidogo na kwenda mwendo wa wastani. Baadaye, alianza kusinzia kidogokidogo na nilipomkumbusha kila mara kuhusu tukio hili aliniambia kuwa yeye huendesha daima kwa mtindo huo wa kuonekana anasinzia. Alinilaumu kwa shinikizo zangu za mara kwa mara na kunishauri nikome jinsi nilivyolikoma titi la mama yangu. Ndipo akaingiza gari shimoni!” Alaa! Njoo tushauriane zaidi chini ya mti.
Maelezo
Kifungu cha hapo juu kimetumia vielezi vya idadi, kiasi na mahali.
(i) Vielezi vya idadi hudhihirisha kuwa kitendo kilitendeka kwa kiasi fulani au mara fulani. Idadi inayotajwa ni ya kujumlisha au kukadiria tu na wala haihesabiki. Kwa mfano: kila mara, mara moja.
(ii) Vielezi vya mahali vinataja dhana ya mahali. Kwa mfano: ndani, nje.
(iii) Vielezi vya kiasi vinakadiria mambo. Kwa mfano: kidogo, kiasi.