Sentensi ni mwambatano wa maneno wenye maana. Usahihi wa mwambatano huo hutegemea sheria za lugha inayohusika. Maneno kwenye sentensi huwa katika mafungu yenye uhusiano wa kimuundo na kimatumizi.
Aina za sentensi
(a) Sentensi Sahili: Hii inalingana na kishazi kimoja, lakini huwasilisha ujumbe uliokamilika. Ni kama kishazi kilichojihimili. Kwa mfano:
- Kijana alimsaidia mzee.
- Walemavu wana haki.
- Ukimwi ni hatari.
- Tunaimba.
(b) Sentensi changamano: Sentensi hii inajumuisha vishazi viwili au zaidi ambapo kimoja hutegemea kingine. Utegemezi huu huashiriwa na vishirikishi tegemezi. Vishirikishi vinavyotumiwa zaidi ni ka, ki, po, nge, ngali.
Kwa mfano:
- Ukimwona mtoto, msaidie.
- Alipokutana na mzazi, aliomba msamaha.
- Wanaougua wanahitaji matibabu.
(c) Sentensi ambatano: Hii hujumuisha vishazi viwili vinavyolingana kimuundo. Hutegemea viunganishi na, au, lakini. Kwa mfano:
- Mwanafunzi alifanya bidii na akapita mtihani.
- Omari alikuwa mkulima au mfanya biashara.
- Nilienda dukani lakini sikufanikiwa.
Kila sentensi hapo juu ina sentensi mbili zinazorejelea nomino moja. Unaweza kuzitambua sentensi hizo? Sentensi za Kiswahili hutegemea virai na vishazi ili kukamilika.
Virai
Kirai: Ni fungu la maneno lisilokuwa na kiima na kiarifu chake. Kumbuka kuwa kiarifu ni yale yanayosemwa kuhusu ‘kitu’ kinachohusika.
Aina za virai
Kuna aina zifuatazo za virai:
- Virai nomino.
- Virai vitenzi.
- Virai vivumishi.
- Virai vielezi.
- Virai viunganishi.
(a) Virai nomino
Mifano:
(i) nomino peke yake:
- dawa zimekwisha.
(ii) nomino mbili au zaidi zilizounganishwa:
- mwalimu na mwanafunzi wanashirikiana.
(iii) nomino na kivumishi:
- mtu mnene amemsaidia maskini.
(iv) nomino na sentensi:
- mzazi aliyempeleka binti yake chuoni amepongezwa.
(b) Virai vitenzi
Mifano:
(i) kitenzi peke yake:
- amesafiri.
(ii) kitenzi na nomino:
- amempeleka Juma.
(iii) kitenzi na kitenzi
- anapenda kusoma.
(c) Virai vivumishi
Mifano:
(i) kivumishi na vielezi:
- baya sana.
- eusi ti ti ti!
(ii) kivumishi na kirai-nomino:
- enye gari kubwa.
(iii) kivumishi na kirai-kitenzi:
- enye kufanya ghasia.
(d) Virai vielezi
Mifano:
- sana sana
- mara nyingine
- juu ya dawati.
(e) Virai-viunganishi
Mifano:
- kwa bibi yake
- kwa miguu
- mwanafunzi katika uwanja.
Vishazi
Kishazi: Ni kundi la maneno lenye kiima na kiarifu, hasa likiwa ndani ya sentensi kuu.
Aina za vishazi
- vishazi-viambatani (huru)
- vishazi vitegemezi.
Vishazi viambatani: Hivi vimeunganishwa katika sentensi kuu na viunganishi, hasa na na lakini.
Vinapoondolewa kwenye sentensi kuu, huwa sentensi zinazojitegemea.
Kwa mfano:
- mhasiriwa alipelekwa hospitali na akatibiwa.
- alicheza mpira vyema na kuisaidia timu yake.
Viunganishi vingine vinavyotumika ni: wala, au, na tena. Kwa mfano:
- sijui wala sijali.
- soma kwa bidii au utafukuzwa.