(a) Nyakati (Njeo)
Nyakati ni kipindi au muda maalum wa kitendo kutokea. Kuna nyakati tatu kuu: Wakati uliopita, wakati uliopo na wakati ujao. Wakati uliopita huwakilishwa na kiambishi -li-, wakati uliopo huwakilishwa na kiambishi -na-, nao wakati ujao huwakilishwa na kiambishi -ta-.
Tazama matumizi ya nyakati hizo katika sentensi zifuatazo:
- Amina a-li-wakaribisha wageni wengi jana.
- Sinzore a-li-toa hotuba kwa Kiswahili.
- Walimu wa chuo wa-na-dai nyongeza ya mshahara.
- Wapishi wa-na-jitayarisha kwa sherehe.
- A-li-sema a-ta-chelewa kidogo kwa kuwa a-na-jitayarisha kusafiri kesho.
- Mgeni mashuhuri a-li-tangaza kuwa a-ta-tutembelea kesho, kwa hivyo tu-ta-mtarajia.
(b) Hali
Hali ni dhana ya wakati ambayo inawakilishwa na viambishi fulani kwenye kitenzi. Viambishi hivi huitwa hali za nyakati. Havionyeshi moja kwa moja wakati ambapo kitendo kinatokea bali hurejelea hiyo dhana ya nyakati.
Ifuatayo ni mifano ya hali za nyakati.
- hu – hurejelea hali ya mazoea.
Kwa mfano: Mtoto hunyonya titi la mamake.
- me – hurejelea hali timilifu. Yaani, kitendo tayari kimekamilika.
Kwa mfano: Bwana Arusi amewasili ukumbini.
- ha – hurejelea hali kutegemea wakati uliomo kwenye sentensi.
Kwa mfano: Mwalimu haji darasani.
- ki – hurejelea hali changamano za vitendo.
Kwa mfano: Alipowasili nilikuwa nikioga.
- nge, ngeli, ngali – hurejelea hali ya masharti yasiyodhihirika.
Kwa mfano: Angeniandikia barua ningejibu.
- Ka-hurejelea hali tegemezi.
Kwa mfano: Kaniombee ruhusa kwa mkurugenzi.
- Po – hurejelea hali inayobainika wakati kitendo kimetimia au kitakapotimia.
Kwa mfano: Tulipowasili tulipewa kikombe cha chai.
- e – hurejelea hali changamano kama vile kuamuru, kutarajia, kusihi au kutia shime.
Kwa mfano:
- Ulie, usilie sikupi pesa zangu.
- Upige, usipige simu sitakujulia hali mimi.
- a – hurejelea hali ya wakati usiodhihirika bayana. Kwa mfano:
(i) Mkulima apenda maharagwe.
(ii) Mwalimu afunza watoto.
Matumizi ya nyakati na hali
- Wakati ujao – hali timilifu
- Gari litakuwa limepita kituo cha Limuru.
- Chakula kitakuwa kimepashwa moto.
- Wakati ujao – hali ya kuendelea
- Wanafunzi watakuwa wakifanya hesabu.
- Ng’ombe watakuwa wakilishwa.