Kama ilivyoelezwa katika sehemu mbalimbali za Tanzu za Lugha, nomino inayotumika huathiri muundo wa viambishi vingi vinavyotokea katika maneno yaliyotumika. Lugha ya Kiswahili, kama lugha nyingine za Kibantu, ina utaratibu wa nomino ambapo muundo wa viambishi vya maneno (vitenzi, vivumishi, viwakilishi, vielezi na kadhalika) huongozwa na aina ya nomino. Kwa mfano:
- Chebii alikuwa mwanamichezo aliyejulikana Afrika nzima.
Nomino ndiyo inayotawala sentensi nzima na huathiri viambishi vinavyohusiana nayo. Vivumishi vya A-Unganifu ni virai vinavyovumisha nomino.
Kwa mfano:
- Suruali ya Moseti
- Jina la Lokorito
Kama ilivyodokezwa hapo juu virai hivi hutegemea ngeli ya nomino.
Kwa mfano:
A: Mtoto wa mama
WA: Watoto wa mama
U: Mlima wa Kenya
I: Milima ya Kenya
U: Ugonjwa wa kifua
YA: Magonjwa ya kifua
LI: Jino la dhahabu
YA: Meno ya dhahabu
KI: Cheti cha uanasheria
VI: Vyeti vya uanasheria
I: Nyumba ya wazazi
ZI: Nyumba za wazazi
I: Hewa ya siku hizi
I: Hewa ya siku hizi
U: Ukuta wa mawe
ZI: Kuta za mawe
U: Ukarimu wa mwalimu
U: Ukarimu wa mwalimu
KU: Kusoma kwa kasi
PA: Pahali pa kupumzika
KU: Kwahali kwa kupumzika
MU: Mwahali mwa kupumzika
Kama inavyodhihirika hapo juu, A-Unganifu inashikamanisha nomino mbili na hubadilika kutegemea ngeli. Wanafunzi wengi husumbuliwa na upatanisho wa kisarufi ilhali ni sehemu muhimu sana ya lugha ya Kiswahili. Mwanafunzi anahimizwa ajitahidi kadri iwezekanavyo ili aimarishe sarufi yake.