SARUFI – MWINGILIANO WA MANENO: KIVUMISHI/KIWAKILISHI

Kufikia sasa, mmesoma vitabu mbalimbali vyenye maelezo tofauti kuhusu vivumishi na viwakilishi.

Katika baadhi ya vitabu vya Sarufi ya Kiswahili, kumekuwa na tatizo la maneno mengine kuainishwa kama vivumishi ilhali yangefaa kuainishwa kama viwakilishi. Kwa mfano, katika kitabu cha Kapinga (1983) kiitwacho Sarufi Maumbo ya Kiswahili, mwandishi ameorodhesha aina hizi za “vivumishi”:

(a) Vivumishi vimilikishi: yake, zao, n.k.

(b) Vivumishi vionyeshi huyu, pale, n.k.

Naye Waihiga (1999) katika kitabu chake Sarufi Fafanuzi ya Kiswahili ameainisha vivumishi katika makundi kumi ifuatavyo:

1. Vivumishi vya sifa k.m. mzuri, mweusi.

2. Vivumishi vya idadi k.m. wengi, wanne.

3. Vivumishi vya kumiliki k.m. yangu, yao.

4. Vivumishi vya kuonyesha k.m. huu, ule.

5. Vivumishi vya kusisitiza k.m. hikihiki.

6. Vivumishi vya pekee k.m. mwenye, yoyote.

7. Vivumishi vya kuuliza k.m. ngapi, gani.

8. Vivumishi vya A-Unganifu k.m. ya Omollo, ya babu,

9. Vivumishi vya kurejelea k.m. huyo, hicho.

10. Vivumishi vya jina k.m. kipofu, shujaa.

Lakini tukichukulia kuwa kivumishi ni kipashio kinachotoa “maelezo zaidi juu ya nomino”, inatudhihirikia kuwa baadhi ya maneno yanayoitwa “vivumishi” na wanasarufi hao ni viwakilishi. Mwingiliano huu wa maneno unatokana na uainishaji. Kwa hakika, tuna aina zifuatazo za vivumishi:

(a) Vivumishi vya sifa

(b) Vivumishi vya idadi

(c) Vivumishi vya kuulizia (vivumishi ulizi )

(d) Vivumishi vya pekee.

Huu ndio uainishaji unaopendekezwa na Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (2001). Uainishaji huu umejikita katika msingi wa maana, wala si maumbo.

Tatizo hili la uainishaji pia linajitokeza kuhusu viwakilishi.

Viwakilishi vinasimamia nomino. Kumekuwa na maoni mbalimbali kuhusu idadi ya viwakilishi. Ashton (1994) ametaja viwakilishi vifuatavyo:

(a) Viwakilishi vimilikishi (pamoja na A-ya uhusiano)

(b) Viwakilishi vionyeshi

(c) Viwakilishi viulizi

(d) Viwakilishi O-rejeshi

(e) Viwakilishi -ote, -o-ote

(f) Viwakilishi -enye, na -enyewe.

Waihiga (2003) ameainisha viwakilishi vifuatavyo:

1. Viwakilishi vya kuonyesha

2. Viwakilishi vya kumiliki

3. Viwakilishi vya kuuliza

4. Viwakilishi vya kurejesha

5. Viwakilishi vya nafsi

6. Viwakilishi vya ngeli

7. Viwakilishi vya pekee

8. Viwakilishi vya idadi

9. Viwakilishi vya A-unganifu

10. Viwakilishi sifa.

Kama itakavyodhihirika, kuna wanasarufi wanaosema viwakilishi fulani ni vivumishi. Uainishaji huu unakanganya. Vivumishi vina nafasi yake katika sarufi ya lugha na hali kadhalika viwakilishi. Kwa hakika viwakilishi vya Kiswahili ni hivi vifuatavyo:

1. Viwakilishi vionyeshi

2. Viwakilishi viulizi

3. Viwakilishi vimilikishi

4. Viwakilishi nafsi.

Mwingiliano wa makundi ya maneno unatokana na uainishaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *