Lugha ya Kiswahili ina vitenzi asilia (kwa mfano: pika, kata, leta) na vya kigeni (kwa mfano: ghairi, samehe, tubu). Vitenzi asilia vina irabu a mwishoni katika hali ya kuyakinisha. Irabu hii ni kiishio na hupatikana katika mwisho wa vitenzi vingi vya lugha za Kibantu, katika uyakinishaji.
Vitenzi vya kigeni vinatokana na mkopo kutoka hasa lugha ya Kiarabu. Mwisho wa vitenzi hivi mara nyingi ni e, i, u na ni sehemu ya mzizi; kwa mfano: starehe, ajiri. Kuna vitenzi vichache vyenye asili ya kigeni vinavyoishia a; kwa mfano: shiba, batiza.
Katika kunyambua vitenzi vyenye asili ya kigeni, kiambishi huambikwa kwenye mwisho wa kitenzi. Irabu ya mwisho inaweza kudondoshwa au kuunganishwa na ya kiambishi.
Tazama mifano ifuatayo:
Tenda | Tendee | Tendesha | Tendeka |
samehe | samehea | samehesha | sameheka |
haribu | haribia | ||
rudi | rudia | rudisha |
Kauli ya kutendeshewa
Kauli hii inatokana na kauli ya kutendesha, kutendea na kutendewa.
Katika kauli ya kutendea, kiambishi kinachotumika ni a kinachotokea mwishoni mwa neno zima, endapo mzizi unaishia i au e. Kwa mfano:
hubiri – hubiria
afiki – afikia
samehe – samehea
starehe – starehea
Endapo mzizi unaishia a, irabu hii hudondoshwa na kuongezewa viambishi i na a mwishoni. Kwa mfano:
adhibu – adhibia
hutubu – hutubia
Udondoshaji wa irabu u hutokana na kaida ya lugha ya Kiswahili isiyoruhusu mkururo wa irabu nyingi zinazofuatana. Lengo ni kurahisisha matamshi.
Kwa mfano:
Endapo mzizi unaishia irabu mbili kama au, huongezewa li pamoja na kiishio a.
sahau: sahau-li-a
dharau: dharau-li-a
Kumbuka kwamba unyambuaji sharti uwe na maana kimantiki. Baadhi vitenzi vya kigeni (na pia vya kiasili) vikinyambuliwa kwenye kauli ya kutenda havileti maana. Kwa mfano, huwezi kunyambua kitenzi ‘balehe’ katika kauli ya kutendea.
Katika kauli ya kutendewa kiambishi kinachotumika ni iw, inayojitokeza kama ew wakati mwingine.
Kwa mfano:
Kitenzi | Kuongeza kiambishi | Kauli |
tafiti | tafiti-iw-a | tafitiwa |
samehe | samehe-iw-a | samehewa |
zidi | zidi-iw-a | zidiwa |
dhihaki | dhihaki-iw-a | dhihakiwa |
Kama inavyodhihirika, irabu moja hudondoshwa ili kurahisha matamshi. Ikiwa mzizi unaishia irabu u, irabu hii hudondoshwa na kiambishi kuongezwa.
Kwa mfano:
Kitenzi | Kuongeza kiambishi | Kudondosha irabu | Kauli |
salimu | salimu-iw-a | salim-iwa | salimiwa |
hukumu | hukumu-iw-a | hukum-iwa | hukumiwa |
jibu | jibu-iw-a | jib-iwa | jibiwa |
Ikiwa mzizi unaishia irabu mbili kama au, kiambishi liw hutumika, ili kuvunja
mkururo wa irabu. Kwa mfano:
sahau | sahau-liw-a | sahauliwa |
dharau | dharau-liw-a | dharauliwa |
Kauli ya kutendesha
Vitenzi hivi vinafuata utaratibu ulioelezwa hapo juu. Ikiwa mzizi unaishia irabu u, irabu hii hudondoshwa na kuongezewa kiambishi ish pamoja na kiishio.
Kwa mfano:
ratibu | ratib-ish-a |
husu | hus-ish-a |
dumu | dum-ish-a |
Tazama mifano hii:
safiri | safirisha |
hakiki | hakikisha |
starehe | starehesha |
Ni nini kinachoendelea? Zingatia maelezo ya hapo juu katika kujibu swali hili.
Kauli ya kutendeshewa
Ni dhahiri kuwa kauli hii itakuwa na kiambishi mwafaka kutegemea aina ya irabu kwenye mzizi. Kwa mfano:
ratibu | ratib-ishiw-a |
hakiki | hakik-ishiw-a |
Kauli ya kutendeana
Utakumbuka kuwa kiambishi cha kauli ya kutendeana ni an.
Kwa mfano:
hoji | hoji-an-a |
karibu | karibu-an-a |
ruhusu | ruhusi-an-a |
samehe | samehe-an-a |
sahau | sahau-lian-a |
dharau | dharau-lian-a |
Zingatia:
Ikiwa mzizi unaishia kwa irabu i tunaongeza kiambishi an pamoja na kiishio a. Ikiwa mzizi unaishia irabu u hudondoshwa na kiambishi i huingizwa, pamoja na an na kiishio a. Mzizi unapoishia e tunaongeza an pamoja na kiishio. Ikiwa mzizi unaishia irabu mbili kama au tunaongeza lian, pamoja na kiishio. Kwa jumla, basi, katika unyambuaji wa vitenzi vya kigeni ni muhimu kuzingatia irabu ya mwisho wa mzizi na namna inavyoingiliana na viambishi vya kauli mbalimbali.