SARUFI: MNYAMBULIKO WA VITENZI

Mnyambuliko wa vitenzi ni nini?

Mnyambuliko wa vitenzi ni utaratibu wa kuunda vitenzi vipya kwa kuongeza viambishi nyambulishi kwenye maumbo ya mizizi. Kwa mfano:

KitenziMnyambuliko
Pig-apig-w-a
pend-apend-an-a
pit-apit-ish-w-a
let-alet-ew-a

Katika mifano hiyo hapo juu, vitenzi vimeongezwa viambishi nyambulishi. Utaratibu wa unyambuaji licha ya kuongeza viambishi kwenye mzizi unatekeleza wajibu mwingine: kila umbo linalonyambuliwa lina maana tofauti ijapokuwa maana hiyo inafungamana na maana ya msingi inayodokezwa na mzizi. Kwa mfano, neno pigwa linaashiria mtu au kitu kufikwa na tendo ilhali pigana lina maana ya kuwahusu watu au vitu viwili ama zaidi. Unyambuaji huongozwa na kauli za vitenzi.

Viambishi vinavyotumiwa katika mnyambuliko wa vitenzi ni vifuatavyo.

KiambishiMaanaMfano
(a) -w-Kitendwapikwa
(b) -ik-/-ek-Kitendekasomeka
(c) -ish-/-esh-/-iz-/-ez-Kitendeshisomesha
(d) -il-/-li-/-el-/-le-/-ili-/-ele-/-i-/-e-Kitendeapikia
(e) -o-/-u-Badilifufungua
(f) -am-Kifungamanishiungama
(g) -at-Kishikanishifumbata
(h) -an-Kitendanishipendana

Kila kiambishi kinaambatana na kauli yake ya kitenzi.

Katika sehemu hii tunashughulikia kauli hizi za vitenzi.

(a) Kutendeshewa

(b) Kutendesheana

(c) Kutendesheka

(d) Kutendama

(e) Kutendata

(f) Kutendua

(g) Kutenduka.

(a) Kutendeshewa

Kauli hii inatokana na mwingiliano baina ya kauli ya kutendesha, kutendea na kutendewa.

Kiambishi cha kauli ya kutendesha ni:- esh-/-ish-/-ez-/-iz-.

Kiambishi cha kauli ya kutendea ni:-i-/-e-

Kiambishi cha kauli ya kutendwa ni:-w-

Kauli ya kutendesha inaonyesha usababishaji wa kitendo ilhali kauli ya kutendwa huonyesha tendo kumpata mpokeaji. Kauli ya kutendea inaonyesha kutenda kwa niaba/manufaa ya mtu. Kauli ya kutendeshewa inaonyesha tendo kumpata mpokeaji kwa namna ya usababisho.

Kwa mfano:

TendaTendeshaTendesheaTendeshwaTendeshewa
somasomeshasomesheasomeshwasomeshewa
komakomeshakomesheakomeshwakomeshewa

Tazama:

• Mzazi alisomeshewa mtoto na mwalimu.

• Wananchi walikomeshewa wezi na serikali.

Katika sentensi hizi, kauli tatu za vitenzi zimehusishwa.

(b) Kutendesheana

• Kauli hii imehusisha kauli tatu: kutendesha, kutendea, na kutendeana.

• Kauli ya kutendesha ina kiambishi: – sh-/-ish-

• Kauli ya kutendea ina kiambishi: -i-/-e-

• Kauli ya kutendeana ina kiambishi: -an-

Kwa mfano:

TendaTendeshaTendesheaTendeshenaTendesheana
somasomeshasomesheasomeshanasomesheana
komakomeshakomesheakomeshanakomesheana

Tazama:

• Wazazi walisomesheana watoto.

Katika sentensi hii kitendo cha kuwafanya watoto wasome kilihusisha wazazi labda kwa kupishana kufundisha au kwa kufaana.

(c) Kutendesheka

Kauli hii inahusisha kauli mbili: kutendeka na kutendesha.

Kumbuka kwamba kauli ya kutendeka inaonyesha uwezekano wa jambo/kitu kutendeka. Kiambishi chake ni -ik-/-ek-.

Kwa mfano:

TendaTendeshaTendekaTendesheka
FumbaFumbishaFumbikaFumbishika
PigaPigishaPigikaPigishika
LalaLalishaLalikaLaLishika

Tazama:

• Mpira huu haufumbishiki kwa sababu ni mkubwa mno.

(d) Kutendama

Kauli hii ni ya ufungamanishi. Inaonyesha kuwa watu, vitu au hali inaambatana au kunasa mahali kwa namna ya msuguano.

Kiambishi cha kutendama ni -am- na hufuata mzizi moja kwa moja.

Kwa mfano:

TendaTendama
fung-afung-am-a
ach-aach-am-a
tung-atung-am-a
gand-agand-am-a

Tazama:

Maziwa yaligandama kibuyuni.

(e) Kutendata

Kauli hii huonyesha mshikano; yaani tendo la kufanya watu au vitu kushikana. Kiambishi cha kutendata ni -at- na hufuata mzizi wa kitenzi moja kwa moja.

Kwa mfano:

TendaTendata
fumb-afumb-at-a
pak-apak-at-a
kam-akam-at-a

(f) Kutendua

Kauli hii ni ya ubadilifu. Huonyesha kuwa tendo ni kinyume.

Kiambishi cha kauli hii ni -o-/-u-.

Kwa mfano:

TendaTendua
Fung-aFung-u-a
Chom-aChom-o-a
Zib-aZib-u-a
Umb-aUmb-u-a

Zingatia kuwa endapo mzizi wa kitenzi una irabu a, i, u, kauli ya kutendua itakuwa na kiambishi u na endapo mzizi una irabu o au e, kauli ya kutendua itakuwa na kiambishi o.

(g) Kutenduka

Kauli hii inajumuisha kauli ya kutendua na kutendeka. Kumbuka kwamba

kiambishi cha kutendeka ni -ik-/-ek-.

Kwa mfano:

TendaTenduaTendekaTenduka
fungafung-u-afung-ik-afung-uk-a
kwamakwam-u-akwam-ik-akwama-uk-a

Kauli za jumla kuhusu mnyambuliko wa vitenzi

Irabu inayotumika katika viambishi vya mnyambuliko hutegemea aina ya irabu iliyoko kwenye mzizi. Kwa mfano, ikiwa mzizi una irabu a, i, u tunapata li kwenye kiambishi cha mnyambiliko na ikiwa mzizi una irabu e na o tunapata e. Katika kauli ya kutendua, endapo mzizi una a, i, u tunapata u na ikiwa mzizi una irabu e na o tunapata o.

Pia sauti I hutumika katika unyambuaji ili kuvunja mfululizo wa irabu. Kwa mfano:

toato-lesh-a
juaju-lish-a.

ZOEZI

Tunga sentensi mbilimbili zinazoonyesha vitenzi vya kauli ya:

(a) Kutendesheka

(b) Kutendata

(c) Kutendua

(d) Kutendama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *