Sajili ni matumizi ya lugha katika mazingira na viwango maalum. Baadhi ya viwango hivi ni kama vile dini, sheria, biashara, michezo na magazeti. Sajili pia hujulikana kama rejesta.
Baadhi ya mambo ambayo hutawala matumizi ya Sajili ni:
(i) Umri wa mzungumzaji/msemaji.
(ii) Cheo au tabaka lake.
(iii) Muktadha au mazingira/hali inayotamalaki.
(iv) Uhusiano baina ya watu.
(v) Mada au hoja inayozungumzwa.
Mtindo unaotumiwa katika kuelezea mambo pia hutupa picha halisi ya yaliyomo. Kwa mfano, matumizi ya sentensi fupifupi katika mazungumzo, matumizi ya sentensi ndefundefu katika sheria, na kadhalika.
Mifano ya Sajili
(i) Sajili ya matangazo ya biashara.
(ii) Sajili ya matangazo ya kandanda/michezo.
(iii) Sajili ya kisheria/mahakama.
(iv) Sajili ya kidini.
(v) Sajili ya magazeti.
(vi) Sajili ya kishairi.
Sajili ya Matangazo ya Biashara
Lugha ya matangazo ya biashara inalenga kutoa habari kuhusu ulimwengu wa biashara unaowakilishwa na huduma na bidhaa mbalimbali. Lengo la matangazo haya ni kuwashawishi na kuwasaidia watu kufanya uamuzi wa busara katika ununuzi. Aidha, wanunue bidhaa fulanifulani kwa wingi.
Sifa za Matangazo ya Biashara
(i) Watangazaji hawajifungi na matumizi ya lugha sanifu. Huwa na uhuru wa kuchanganya ndimi, kutumia Kiswahili ‘kibaya’ ili kuwavutia wateja wa kawaida ambao ndio wengi.
Kwa mfano:
Hei, hei biashara haigombi
Huna bahshishi yahe?
Sabuni ya Ng’arisha ni ya kishua.
(ii) Lugha ya matangazo ya biashara imejaa porojo na chuku. Lengo huwa kuwashawishi watu wanunue bidhaa au huduma fulani mahsusi.
Kwa mfano:
Dawa ya Power ina nguvu ya kumfanya mzee ajihisi kama kijana wa miaka kumi na saba. Usizeeke. Inunue sasa.
(iii) Pia, kuna ubembelezi unaotumia picha za warembo wazuri, muziki mwororo au watu mashuhuri waliofaulu maishani.
Kwa mfano:
Daktari Kipchoge Keino anatumia viatu vya Njumu. Je, wewe una vyako?
Matumizi ya muziki na warembo huwavutia watu wengi, hususan vijana ambao idadi yao, mara nyingi, hushinda wazee.
(iv) Lugha huwa nyepesi na rahisi kueleweka. Lengo ni kutoa ujumbe kwa njia ya moja kwa moja na kwa uwazi.