Muhtasari au ufupisho ni mbinu muhimu sana katika taaluma ya uandishi. Ni uwezo wa kueleza maana iliyomo katika habari kwa kutumia idadi chache ya maneno, bila kupotosha maana ya makala asilia. Muhtasari huchuja mambo muhimu yanayohitajika katika makala hayo. Lengo kuu la kufupisha ni kupunguza urefu au kueleza kwa maneno machache kuliko yale yaliyotumiwa katika makala asilia. Yaani, muhtasari ni kiwakilishi kifupi cha makala marefu.
Baadhi ya hoja muhimu katika mukhtasari
- Mwandishi anazungumzia mada gani? Kwa mfano: ukulima, uvutaji sigara.
- Ni mawazo gani, kwa ujumla, yanayohusika katika makala yanayofupishwa?
- Ni mambo muhimu yapi yanayofaa katika kila aya?
- Mwandishi ametumia mtindo upi katika uwasilishaji wake, kwa mfano, maelezo mfululizo, hotuba, n.k.
Sifa za Mukhtasari bora
- Uzingatifu wa mambo muhimu yanayobainika.
- Kuyaunganisha mambo muhimu kimantiki.
- Muhtasari uwe unaotiririka na unaoumana.
- Taarifa iliyofupishwa isiwe na mifano au maelezo ya ziada.
- Matumizi ya msamiati mkomavu unaojumlisha mawazo kadha kwa pamoja.
- Muhtasari uzingatie mpangilio wa taarifa asilia ili ujumbe usipotoshwe.
- Maneno na hati zisomeke kwa urahisi. Pasiwe na utatanishi wowote.
- Mfupishaji asiongeze maoni yake binafsi ambayo hayakujitokeza katika makala asilia.
- Taarifa iliyofupishwa ijitokeze kwenye aya moja ya takriban maneno thuluthi moja (1/3) ya makala asilia. Mara nyingi, idadi ya maneno yatakayotumiwa huwekwa kwenye mabano baada ya kila swali.
Hatua za kuandika Mukhtasari
(i) Soma na kuelewa barabara mawazo yaliyomo katika makala asilia. Makala yasomwe kimarudiomarudio ili msomaji awe na hakika kwamba ameyaelewa.
(ii) Tenganisha hoja muhimu kutoka kwa maelezo ya ziada.
Zivunjevunje na kuzipanga katika vijisehemu/vidokezi.
(iii) Tambua maana husishi ya kila neno ili uache kurudiarudia hoja moja.
(iv) Tayarisha mswada sawidi kutokana na vidokezi hivyo, bila kurejelea kazi asilia.