METHALI ZA KISWAHILI

Maana ya methali

Methali ni kifungu cha maneno yenye hekima yanayotumiwa kimafumbo katika kuwaelekeza wanadamu. Methali zimejikita katika mila, desturi, mazingira na kazi za wanajamii.

Methali nyingi za Kiswahili, kwa mfano, zinarejelea bahari, uvuvi, ukulima na ufugaji. Hii ni kwa sababu chimbuko la Kiswahili ni pwani ya Afrika Mashariki penye kazi hizo za kijadi.

Baadhi ya methali zinazoongelea bahari na uvuvi ni kama vile:

  • Mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani.
  • Avumaye baharini papa, kumbe wengine wapo.
  • Wavuvi wa pweza hukutana nyambani.
  • Msafiri ni aliye pwani.

Uamilifu wa Methali

Methali ni muhimu katika maisha ya binadamu kwa njia zifuatazo:

(i) Kuhifadhi mapisi (historia), mila na desturi za watu.

Kwa mfano:

  • Mpemba hakimbii mvua ndogo.
  • Mgala (kabila adui) muue na haki umpe.
  • Ada ya mja hunena mwungwana ni kitendo.

(ii) Kukuza na kuendeleza ufasaha wa lugha. Yaani, takriri ya silabi.

Kwa mfano:

  • Mkata haendi mkele, akienda mkele hujaza mchele jahazi tele, hurudi na upele.
  • Mkata (maskini) akipata matako hulia mbwata.
  • Toma kwa toma hazitomani.

(iii) Kuwaelekeza, kuwafunza na kuwaadilisha wanajamii.

Kwa mfano:

  • Akutendaye mtende, mche asiyekutenda.
  • Kazi mbi si mchezo mwema.
  • Penye itifaki, ikrahi haipiti.
  • Akufukuzaye hakwambii toka.
  • Aliye kando haangukiwi na mti.
  • Mtego wa panya hunasa waliomo na wasiokuwemo.

(iv) Kuwatanabahisha au kuwazindua watu.

Kwa mfano:

  • Kikulacho ki nguoni mwako.
  • Akumulikaye mchana, usiku akuchoma.
  • Aliyekutangulia chanoni hukuzidi kwa tonge.

Nduni (Sifa) za Methali

Methali za Kiswahili zina nduni mbalimbali. Baadhi yazo ni:

(i) Matumizi ya lugha ya kiistiari au picha.

Kwa mfano:

• Dunia mti mkavu, kiumbe siulemele.

(ii) Matumizi ya lugha ya kishairi.

Kwa mfano:

  • Ajaye kisimani mbele hunywa maji maenge. Hayawi! Hayawi! huwa.
  • Gonga gogo usikie mlio.
  • Atangaye na jua hujua.

(iii) Matumizi ya sifa za kinyume au kupingana.

Kwa mfano:

  • Aliye juu mngojee chini.
  • Mpanda ngazi hushuka.
  • Wagombanao ndio wapatanao.

(iv) Matumizi ya kiulizi na jawabu.

Kwa mfano:

  • Mtaka cha mvunguni (hufanya nini?) – sharti ainame.
  • Cha mlevi (hufanywa nini?) – huliwa na mgema.

(v) Matumizi ya tamathali za usemi changamano. Kwa mfano:

  • Jambo usilolijua ni usiku wa giza (stiari).
  • Nazi haishindani na jiwe (stiari).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *