MATUMIZI YA LUGHA KATIKA KAZI ZA SANAA

TAMATHALI ZA USEMI

Tamathali za usemi ni mtindo wa kutumia lugha kwa ustadi kwa makusudi ya kupamba kazi ya sanaa. Aidha, fungu la maneno huteuliwa na kutumiwa na mwandishi kwa lengo la “kufananisha” kinachoelezwa na hali au kitu fulani maishani. Neno ‘tamathali’ lina maana ya ‘kufananisha’ au ‘kulinganisha’ (mithilisha).

Malengo ya kutumia tamathali za usemi

  • Kueleza nia kamili ya mwandishi, kwa mfano: kufanya mzaha, kufurahisha, kuhamasisha, kufunza na hata kumfanya msomaji aichukie tabia au nafsi fulani.
  • Kustawisha na kudumisha lugha: lugha ni chombo hai kinachozidi kukua mchana na usiku. Kwa mfano, kuna semi za msimu zinazoingizwa katika lugha na kuiathiri vilivyo. Baadhi ya semi hizi hushika na kutanua msamiati wa lugha yenyewe.

Mifano ya tamathali za usemi

(i) Balagha:

Ni mbinu ya kutumia maswali ambayo hayatarajiwi kupewa majibu papo hapo. Balagha humsaili msikilizaji au msomaji kwa kuingilia hisia zake za ndani na kumfanya aibue maoni yake kwa kutenda atakachoamua kutokana na huko kusailiwa.

Mfano:

Ikiwa ulijua huna pesa, kwa nini uliniambia nizijie leo? Unafikiri mimi ni mtoto wa kuahidiwa kila uchao?

(ii) Tashbihi:

Ni maneno yanayofananisha (au kushabihisha) kitu, jambo au kitendo na kingine kwa kutumia vihusishi kama; ja, mithili ya, n.k. Tashbihi zinafichua uwanda ili tufahamu zaidi kuhusu vitu vinavyolinganishwa.

(iii) Tashhisi:

Ni kuweka uhai katika vitu visivyokuwa na uhai ili vipate hisia za kibinadamu.

(iv) Majazi:

Ni kumpa mtu jina linalolingana na sifa, matendo au tabia zake.

(v) Jazanda:

Haya ni mafumbo ambamo ndanimwe maana ya kitu imejificha. Ni sawa na stiari, yaani, ‘kilichositiriwa’. Ni uhamishaji wa sifa za A kwenda kwa B. Katika kujadili kuhusu jazanda, tunazingatia mfanano na tofauti baina ya vitu vinavyolinganishwa. Ina uhusiano mkubwa na utamaduni na muktadha wa matumizi.

(vi) Chuku:

Ni kutia chumvi kwa minajili ya kuathiri hisia.

(vii) Tasfida:

Ni kutumia lugha safi (iliyochujwa) ili maneno machafu au yanayoudhi yasitumike. Kwa mfano, badala ya kusema “fulani ana mimba” unasema “fulani ni mja mzito”. Usemi wa pili ni tasfida.

(viii) Taswira:

Taswira ni picha anazozipata msomaji au msikizaji baada ya kusoma, kuona au kusikiliza kazi ya fasihi. Picha hizi huwa zina funzo fulani. Ili kujenga taswira, mtunzi mara nyingi hutumia tamathali mbili za usemi: jazanda na tashbihi.

(ix) Taharuki:

Taharuki ni mbinu inayotumiwa na watunzi wa kazi za kubuni ili kuteka nadhari na hamu ya wasomaji. Ili kujenga taharuki, mtunzi husuka matukio yenye mshikamano na kutiririka kwa muwala ambao unamfanya msomaji asiitue kazi hiyo hadi kikomo chake.

(x) Mbinu rejeshi:

Mbinu rejeshi, ni mbinu ya kisanaa ambapo mtunzi hurudia mambo yaliyokwisha simuliwa awali kupitia mpangilio wa matukio ya kazi au uzungumzi nafsia wa wahusika. Usimulizi wa matukio yakienda nyuma na mbele, huku mwandishi akitumia mbinu hii na mbinu ya viangaza mbele, huzua ploti kioo. Mbinu hii ni kinyume cha mbinu ya viangaza mbele ambapo badala ya kubashiria yatakayotokea baadaye, hurejelea mambo yaliyopita. Kama viangaza mbele, mbinu rejeshi hutumika kufuma matukio mbalimbali katika ploti.

(xi) Viangaza mbele:

Viangaza mbele au kwa majina mengine, “viona mbele” au vibashiria, ni vidokezo ambavyo huwapa wasomaji fununu ya yale yangetokea baadaye katika kazi za kubuni. Mbinu hii, kama mbinu rejeshi, huchukua nafasi muhimu katika ploti ya kazi ya kubuni, hasa, inapounganisha matukio mbalimbali na kubashiri maafa au mambo ambayo yangewafika wahusika baadaye.

(xii) Taashira:

Ishara ni kitu ambacho husimama kwa niaba ya kingine. Yaani, kitu fulani huashiria kitu kingine. Kwa mfano, lugha huundwa na ishara mbalimbali ambazo hutoa maaana tofauti tofauti. Rangi ya kijani kibichi mara nyingi husimamia amani ilhali rangi nyekundu huashiria hatari. Ishara zinaeleweka katika muktadha wa kitamaduni.

Tags: 3259

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *