Shairi la Kwanza
Madawa ya Kulevya
1
Kwa fadha nasikitika, kuwaeleza bayana,
Machozi yananitoka, kufikiria vijana,
Ulevi wamejitwika, sio leo sio jana,
Kwa pamoja tuungane, tuyakatae madawa.
2
Kumi Kumi kumimina, wamefanya ni ibada,
Si wazee si vijana, wamefanza ndio ada,
Ya Muumba meyakana, meyakosea faida,
Kwa pamoja tuungane, tuyakatae madawa.
3
Madawa’yo kwa idadi, maradufu yamezidi,
Umma umeshashitadi, na kufanya ukaidi,
Ya ibura yamezidi, madawa yameshadidi,
Kwa pamoja tuungane, tuyakatae madawa.
4
Hashishi na kokenia, sio jambo la ajabu,
Ingawaje ni tanzia, na kitu kiso adibu,
Taabuni kujitia, madhila yametusibu,
Kwa pamoja tuungane, tuyakatae madawa.
5
Kilio kimetukumba, wanetu ‘meangamia,
Madawa yamewabeba, ‘mewaghururi dunia,
Staha mewaambaa, na hadhi kujishushia,
Kwa pamoja tuungane, tuyakatae madawa.
6
Kaditama nakingama, sendi mbele wala nyuma,
Yalo mema nimesema, sidhani mtalalama,
Namuombeni Karima, atuepushe salama,
Jamanini tuungane, tuyakatae madawa.
(Salim Swaleh, 2003)
Shairi la Pili
Sigara
1
Sigara kitu dhaifu
Madharake maradufu
Hukufanya uwe mfu
Hukupora utukufu
Kwenu, wachanga ni rafu
Hujitwika hu uchafu
Afadhali ule dafu
Ubaki mtu nadhifu
Kibwagizo:
Sigara sikupi nafasi
Nafsi yangu unajisi
Maisha yangu ni almasi
Kuipata si rahisi
2
Sigara ‘futa heshima
Huzidisha na gharama
Hushusha yako adhima
‘Kabaki bila karama
Maulana alalama
Watoto wape hekima
Ya kupinga wima wima
Huo moshi wa kuchoma
(Kibwagizo)
3
Sigara sawa laana
Sioni yake maana
Haina hata dhamana
Hufyeka yote hazina
Nawaita kwa mapana Vijana wote kungana Nia iwe kushikana
Masigara kuyakana (Kibwagizo)
4
Tamati Sigara duni Wavutaji ni Wahuni
Tabia zao ni ngeni Si wetu utamaduni
Tuikatie rufani
Sigara ‘siwe thamani
Uwe mwisho maishani
Isivume duniani.
(Kibwagizo)
(Abdul Fatahou, 2003)