Malumbano ya utani ni utanzu wa vichekesho katika fasihi simulizi. Jamii za Kiafrika zina tafrija mbalimbali zinazojumuisha furaha na vichekesho nyingi kama njia mojawapo ya burudani miongoni mwa wanajamii. Lakini katika vichekesho hivyo kuna mafunzo tele.
Kutaniana huku hutokea katika mihadhara ya pombe, ngomani, hafla nyingine kama vile matangani, harusini na kwingine kwingi. Mazingira ya utani huu yanaeleweka vizuri na wahusika na hayatarajiwi kumdunisha au kumdharau anayetaniwa. Ndiposa tukawa na msemo, “watani wa jadi.” Vijana wa mitaani hutumia neno “mchongowano” kwa maana ya malumbano ya utani.
Mifano ya Malumbano ya Utani:
(a) Kisa cha Vayokha (Khayega, Kakamega)
(Mama amekwenda mjini kumtembelea bintiye. Amevumilia “vituko” vya bintiye vya kumlisha majani mabichi na mayai yasiyoiva vizuri kila siku. Anajijasirisha kumwelekeza).
Mama: Mwanangu, unanishangaza sana.
Binti: (Kwa mshangao) Vipi mama?
Mama: Elimu yote niliyokupa nyumbani imepotea bure.
Mbona waniaibisha hivi?
Binti: Bado sikuelewi, mama.
Mama: Umekuwa Muyokha? Vipi unanipa mayai mabichi ninywee chai?
Mimi nilikufunza vizuri sana. Usiniletee Uyokha hapa.
Binti: (Akiangua kicheko) Basi mama, pole sana, nimekuelewa.
Huko nyumbani ulinifunza kupika mboga na mayai kwa muda mrefu sana. Huko ndiko kuharibu vitamini na madini katika chakula. Mboga za majani zimekusudiwa kuliwa mbichi.
Mama: Aka! Nauliza tena umekuwa Muyokha?
Binti: Ni heri uniambie tabia za Wayokha nipate kujigeza kamili.
Mama: Naam, Muyokha ni mtu wa vituko. Kuku wake akitaga yai, yeye hulipanda shambani lipate kumea. Vilevile, hupanda dagaa wamee, Mvua ikianza kunyesha, Muyokha hukunja mwavuli wake usinyeshewe. Baiskeli yake ikipata panchari, aibebe na kuikarabati mbali na pahali ilipoharibikia, yeye huibeba mgongoni tena hadi palepale ilipoharibikia ndipo aipande upya na kuendelea na safari yake. Akinunua beseni, huiweka maji na kuanza kuyachemsha kwenye jiko la kuni au makaa. Na…
(Binti anazidi kucheka na kuomba maji ya kunywa).
Mama: (Kwa utani) Yatakusakama, mwanangu. Mwenyewe ulitaka kujua tabia za Wayokha.
FUNZO: Tufanye mambo kwa kiasi na ustaarabu.
Pia, tujifunze maarifa ya kisasa (hasa kuhusu vitamini na madini).
(b) Kisa cha Mjomba (Mombasa)
(Kijana Juma alimwendea mjombake kwa ushauri kuhusu kumtafuta mchumba).
Juma: Mjomba nipe mawaidha. Nimchague mchumba yupi?
Mjomba: Nitajie wale unaowatarajia.
Juma: Wa kwanza ni Asha, msichana wa Magharibi.
Mjomba: Huyo usimtaje. Watu wake wanaamini kuwa wanamiliki ng’ombe wote duniani. Utatozwa mahari ng’ombe mia moja (vicheko).
Juma: Wa pili ni Pati, msichana wa Mashariki.
Mjomba: Mawee! Kijana umepotea. Watu wa kwao hupenda kula chakula kupindukia. Watakuacha umewamba.
Usikaribishe kijiji kizima nyumbani kwako (vicheko).
Juma: Basi mjomba, nakupa Megi, msichana wa Kusini.
Mjomba: Nakuhurumia sana kijana. Uchawi na wizi utapeleka wapi? Wanao wataishia gerezani bure bilashi (vicheko).
Juma: Sasa mjomba hutaki nioe kabisa?
Kizazi chenu kitaendelea vipi?
Nimemsaza Mwanaidi mrembo wa Kaskazini.
Mjomba: Kijana sikutamaushi lakini Wakaskazini ni wazembe kupindukia. Wanafanyiza upuuzi kama kupoesha uji kwa kutumia gambuti, wanatematema mate ovyo sebuleni. Nyumba yako itakosa ustaarabu na heshima. Katu usithubutu (vicheko).
Juma: Mbona sikuelewi mjomba? Mkeo ni Mkaskazi na naona nyumba yako i nadhifu ja ikulu ya Rais. Niachie uamuzi, ami! (Juma anaondoka).
FUNZO: Usifuate ushauri wa jamaa zako kiholela. Jiamulie hatima