MAHOJIANO NA DAYALOJIA

Ni nini tofauti baina ya mahojiano na dayalojia? Katika mahojiano, anayehoji huuliza maswali na anayehojiwa hujibu. Lengo ni yule anayehojiwa kutoa maelezo kulingana na maswali anayoulizwa. Ili mahojiano yafanikiwe ni muhimu yule anayeuliza maswali atumie lugha ya wazi. Anayejibu anapaswa kufahamu swali (anaweza kuuliza ufafanuzi akitaka) na ajibu kama alivyoulizwa.

Dayalojia ni mazungumzo au majibizano baina ya watu wawili au zaidi. Dayalojia inaweza kuwasilishwa kimazungumzo au kimaandishi.

Mwandishi wa dayalojia anapaswa kufahamu mada anayoiandikia, kutayarisha na kupanga mawazo kimantiki na kimtiririko, na kufikiria wahusika na majukumu yao. Mhusika mfanyabiashara, atatumia lugha tofauti na mhusika mkulima.

Katika dayalojia tunazingatia mambo yafuatayo:

(a) Kutoa maelezo ya ufafanuzi katika mabano ili kufahamisha mambo yanayoendelea.

(b) Kuwa na mazungumzo ya mkato. Mhusika mmoja asitawale mazungumzo mno.

(c) Kutumia vihisishi kama Lo! Kweli! Aah! ili dayalojia isisimue.

(d) Pawe na mwingiliano wa mazungumzo ya wahusika na kudakia maneno ili dayalojia iwe na uhalisi.

(e) Maelezo ya mtunzi kuhusu kinachoendelea yazingatie sarufi. Lugha ya wahusika itegemee shughuli walizopewa.

Mfano:

(Kipruto anaongea na Khelef mtaani)

Kipruto: Khelef, mwaka huu umekuwa mzuri!

Khelef: Si ajabu! Unavyotabasamu ni kama umeshinda bahati nasibu.

Kipruto: Bahati nasibu ya wapi? Mwenzio nimefaulu!

(Anaruka kwa furaha).

Khelef: Umefaulu? Ulikuwa unahojiwa?

Kipruto: Ehe! Nimepokea barua ya kuajiriwa kazi! (Anatabasamu).

Khelef: Hongera Kipruto. Ama kweli mchumia juani.

Kipruto: Ndio, hulia kivulini. Hii ndiyo zamu yangu. Wee! Watanichoka!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *