Misimu ni semi ndogo ndogo za mpito zinazotumiwa katika mazingira fulani kisha kufifia baada ya mazingira yale kutoweka. Aidha, semi za misimu hujitokeza kama tamathali za usemi na zinatofautiana kimaeneo. Kwa mfano, misimu ya Tanzania huenda ikatofautiana na misimu ya Kenya, Uganda au Rwanda. Tazama mifano zaidi ya misimu katika “dondoo” kwenye Taifaleo, Kasheshe na Nipashe.
Mifano ya Misimu
(i) Serikali yetu mpya haikubali mtindo wa kutoa chai ili mtu ahudumiwe katika ofisi za umma. (yaani, kutoa hongo au mlungula).
(ii) Mdosi yule anapenda ndogo ndogo wa mtaani (‘mdosi’ ni tajiri; ‘ndogo ndogo’ ni msichana).
(iii) Soja alisema nimchotee chai. (Askari au mlinzi alisema nimpe hongo/rushwa).
(iv) Mbona mshikaji wangu anataka kunisaliti? (‘mshikaji’ ni mpenzi).
(v) Changudoa amembana tajiri mmoja, hajijui hajitambui. (‘Changudoa’ ni kahaba).
Tahadhari: Shen’g ni kijilugha cha vijana kinachokusudiwa kuwatambulisha kama kikundi maalum. Hubadilikabadilika kutegemea mazingira na msimu. Misimu ni semi za muda lakini si kijilugha kamili. Misimu hujitokeza katika lugha ya kawaida na hubadilika au kutoweka muda huo ukishapita.