Maghani ni kipera cha fasihi simulizi kinachojumuishwa katika fani ya ushairi-simulizi. Kughani ni kitendo cha kusema kwa njia ya mahadhi (kuimba). Mashairi haya yana mdundo wa kishairi na hutoa mapigo yake, usemi baada ya usemi.
Katika jamii nyingi za Kiafrika, watunzi hushindana kughani huku wakitumia lugha iliyopambwa. Ni ushairi unaowasilishwa kwa majinaki na madaha. Kwa mfano, muziki mwingi wa vijana weusi wa Marekani unaghaniwa huku wachezaji wakiinua mikono yao kwa mahadhi ya wimbo. Hali kadhalika muziki wa Marehemu E-Sir (Issa), Nameless (David Mathenge), Poxi Presha, Nazizi na Wahu ni wa kimaghani.
Muziki huu wa vijana umepaliliwa na maghani ya kijadi. Kwa mfano, katika nchi za Afrika Magharibi kuna ushairi wa maghani ujulikanao kama “Jeli”. Miongoni mwa Wamaasai kuna “Eoko,”. Wakikuyu wana “Gicandi” na Wanyarwanda wana “Ibisigo”. Maghani haya ni ya kale na mengine hayaghaniwi tena.