Lakabu ni jina ambalo mtu hujipa au hupewa, mbali na jina lake halisi kutokana na umaarufu fulani au hali ya kutaniana. Lakabu huwa jina la kupanga.
Katika utamaduni wa Waswahili, kwa mfano, washairi wamezoea kujipa majina ya kupanga kama njia mojawapo ya kujisifu na kuwatisha wapinzani wao. Baadhi ya washairi mashuhuri waliojipa majina ya kilakabu kama njia ya kujinaki (kujisifu) ni:
• Ahmad Nassir ni “Ustadh Bhalo” (mtunzi wa Malenga wa Mvita.)
• Hassan Mwalimu Mbega ni “Ustadh Shuara”
(Mtunzi wa Ufupisho wa Malenga; Dafina ya Malenga, n.k).
• Boukheit Amana ni “Ustadh Mti-Mle”, yaani “mti mrefu zaidi kushinda miti mingine (washairi)”. Ni mtunzi wa Malenga wa Vumba.
Aidha, lakabu ni mbinu ya lugha inayotoa sifa ya kipekee au isiyo ya kawaida katika kuelezea hisia au vitendo vya watu au vitu. Kwa mfano, si jambo la kawaida kuona mti mmoja tu msituni ukiwa mrefu zaidi kushinda miti yote.