KUANDIKA TAHARIRI

Tahariri ni taarifa inayochambua mada mahsusi kwa kina. Aidha, huandikwa kwa lugha ya ushawishi na huzingatia mada. Lengo huwa ni kumfanya mtu abadilishe msimamo wake kuhusu jambo fulani. Lugha yake imechujwa na aya ni fupifupi.

MFANO WA TAHARIRI

Serikali Sharti Itwae Ardhi

Harakati za kupambana na unyakuzi wa ardhi haziwezi kufaulu huku wananchi wengine, hasa viongozi, wakiendelea kuteta kuwa Serikali inawaonea licha ya kupatikana walihusika katika kashfa hizo.

Na jinsi hali ilivyo, inaelekea kuna wananchi wengine ambao wako tayari kufa wakijaribu kuhalalisha unyakuzi wao wa ardhi, ikiwemo hata kupambana na Serikali kwa udi na uvumba kuzikinga kutwaliwa. Je, unyakuzi wa ardhi za umma, hifadhi za ujenzi wa barabara, ama mashamba ya wananchi wengine kibinafsi, ni halali? Ni nini sheria inavyosema kuhusu hati za umilikaji wa ardhi zilizonyakuliwa? Je, ardhi zilizonyakuliwa zinaweza kuharamishwa?

Si ajabu kwamba wanyakuzi wengine, wakiongozwa na baadhi ya wabunge na viongozi, wameudhika na habari kwamba Serikali itabomoa majengo yote katika ardhi za hifadhi za barabara mbali na kuwatimua katika mipango ya makao.

Isitoshe, wabunge wengine wanachochea wananchi wasiunge mkono Serikali katika juhudi zake za sasa za kuokoa ardhi zilizonyakuliwa.

Serikali haina budi kuwaambia wanyakuzi hawa wazi wazi kwamba ni lazima warudishe ardhi hizo, na ikiwa wamezistawisha tayari, wabomoe majengo yao. Ni vyema pia kwamba Waziri wa Ujenzi na Barabara, amewaambia wazi wazi kuwa hakuna ridhaa.

Ni juu ya Serikali sasa kuonyesha ina “meno ya kuuma” kwa kutwaa ardhi zote zilizonyakuliwa ikiwa inataka kukomesha wanyakuzi. Hakuna haja kuwaonea huruma kwani wengi wao wanajua kwamba ardhi hizo wanazodai, si zao, bali ni za unyakuzi.

Mipango ya makao, hasa iliyokusudiwa kusaidia wananchi wasio na mashamba na maskwota, imenufaisha matajiri pekee, jamaa zao na marafiki, na yamkini hata baadhi ya wabunge hao wanaoteta. Na Serikali haipasi tu kuokoa ardhi zilizotengewa barabara, zile zilizonyakuliwa misituni na mipango ya makao, bali pia ardhi zote za umma ambazo zimo mikononi mwa wanyakuzi. Hadi sasa, Wananchi hawaamini Serikali itakomboa ardhi hizo, hasa kwa sababu kuna viongozi wake kadha wanaomiliki ardhi walizonyakua. Ni afadhali hata wao warudishe ardhi hizo na majengo yao yabomolewe.

Tags:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *