Insha ya kitaaluma inatakikana iwe dhahiri, iliyolenga mada inayoshughulikiwa na rahisi kufahamika. Insha ya aina hii inapaswa kuwa na mtiririko wenye mantiki. Kwa mfano, unapotoa maelezo kuhusu jumba refu la kimataifa kama la K.I.C.C mjini Nairobi, toa ufafanuzi wako kuanzia orofa ya chini kwenda juu. Ukichanganya maelezo yako bila kufuata mantiki yoyote hutafahamika ipasavyo. Sharti insha ya kitaaluma iwe na muwala na mshikamano. Insha yenye muwala ina mawazo yaliyopangwa hivi kwamba mantiki yake ijidhihirishe. Ikiwa unaandika insha ya kitaaluma inayotegemea sana mawazo ya watu wengine na uyanukuu mawazo hayo, unapaswa kutaja ulikoyatoa mawazo haya. Tena, baada ya kumaliza makala andika marejeleo kamili. Tazama sentensi hii:
“E. Bertoncini (1985) amesema kwamba umefika wakati wa kaumu ya wasomi wa fasihi hasa ya Uzunguni, itambue kwamba fasihi, hasa katika uwanja wa nathari, imefikia viwango vinavyofanana na vile vya kazi za namna hiyo huko Ulaya…………..
Sentensi hii inaonyesha namna makala ya kitaaluma inaweza kuandikwa. Jambo la muhimu katika insha za aina hii ni kwamba mawazo yanapasa kutiririka kimantiki na lugha iwe imechujwa ili iweze kuwasilisha maana inayokusudiwa.