HADITHI FUPI: KIPENDACHO MOYO NI DAWA

Wasitara hasumbuki, wa mbili havai moja Kidawa.

Baba na mama hawakukutakia heri pale walipotaka kukuoza Dau, mwanamume mkofu, mchafu, hakika hakukustahilia. Lo, yasini! Si Kidawa wewe. Unajiona leo ulivyotononoka? Dunia yote ni yako. Moyo maluuni wa Kidawa ulimpa nguvu kwelikweli.

Unajua kwa nini Kidawa akahisi hivyo? Ngoja nikueleze basi. Alikuwa akifurahia maisha yake mapya, baada ya kula arusi miezi michache iliyopita. Arusi yao ilisibu kwa kila kitu na mpaka leo watu wanapohadithia arusi zilizoongoka pale Mlandege, ya Kidawa na Idi ndiyo iliyokuwa ikipigiwa mfano. Arusi si kitu. Maisha baada ya arusi ndiyo aliyokuwa akiyatazamia Kidawa, hasa kwa vile amegombana na wazee wake kwa kumfuata Idi. Lakini ishara zote zilikwisha onyesha kwamba yeye ndiye mshindi, na lile walilotaka wazee wake litokee baina yeye na Idi halikutokea, wala halitatokea.

Kama Kidawa hakuolewa na Idi angaliolewa na nani dunia hii? Sasa dunia yote imekuwa pepo kushinda pepo. Kipi anachokitaka asichokitaka asichotimiziwa? Idi alikuwa maridhia na yeye alijisabilia kwake. Sasa hivi aliingia Idi nyumbani kwa moyo mkunjufu na furaha kama mtoto mchanga. Akenda moja kwa moja mpaka pale kwa mkewe, akamkamata kidevu, akamwangalia, “Kimwana mbona umenuna? Au nd’o unafikiri kwenu ‘vyo?”

“Ukiniambia hivyo Idi naona kama unanisimanga. Mimi sikukufikiri kwetu jana, pale nilipokuwa hawara, nije nikufikiri leo nimeshakuwa mkeo halali yako? Upweke tu, upweke nd’o ulionifanya niwe mnyonge hivi. Idi, umeshanizowesha kuwa na we’ pachapacha. Basi ikipita dadika tu bila ya kukuona, roho yangu hunipaparika. Na leo ya tatu naona mpenzi wangu unachelewa kurudi. Juzi ulirejea saa tatu, jana saa nne, leo saa ngapi sasa?”

“Ass, ni hilo tu mke wangu? Basi mimi mchumi si lazima niwe na uhuru zaidi wa kutoka nje? Na ukitazama sana nakwenda wapi? Si hii mikutano isiyokwisha, leo hili, kesho lile. Lakini kama hilo linakughasi, basi bibi yangu sitatoka. Nisije nikakughasi b’re, na wewe unajua mimi sipendi kukughasi.”

“Ass, si kama naghasika, a-a! Ila hunyongeka, kwani Idi mimi siwezi kuwa mbali nawe hata kwa nukta moja. Lakini sasa nimefurahi kukuona.”

“Si hayo basi kimwana, leo uko mchezo mzuri s’nema, utakaoanza saa sita za usiku. Na ilivyokuwa leo ni Jumamosi, natumai utafurahi kwenda kuuangalia, unaitwa… David and Lucy. Ni mchezo wa mapenzi ya ajabu.

“Nitafurahi kwenda. Na hivi n’nakwenda kujitayarisha.”

Ulikuwa muda mrefu toka Kidawa kutengana na wazee wake. Wametengana, wametupana, hawapitiani wala hawajaonana kwa muda wa miaka miwili. Ilikuwa hasama ambayo haikuwastahilia hata kidogo; lakini waliona bora kushindana na kuvutana. Kila mmoja anaona uzito kwa upande wake kurejea kwa mwenziwe. Baba na mama wanasumbuliwa na ari ya uzee wao kwa kitoto walichokizaa huku wanakwenda mbio. Kwa nini kiwaaibishe? Kwa siku za mwanzo kila upande ulishukuru kuondokewa na mwingine. Walichagua pamoja kufarikiana kama mbingu na ardhi.

Siku moja mama yake alimfungia kibwebwe. Akamkamatia kiuno na kumtolea kidole. Akamkatia wazi, “Nenda mwana kwenda, wamekwenda wangapi na dunia haikugeuka, itakuwa wewe? Labda usiwe mtoto niliyekukopoa miye wewe. Utakuja hapahapa, uje ukamate miguu ya kizee chako. Utarudi, utarudi kama Kaskazi iendayo na kurudi … utarudi na mimi nikusimange kuwa mbona umerudi kwenye ufukara uliokulea wewe mpaka ukakua: shii, nya, ugonjwa, uzima……Leo umekuwa Kidawa mwanamke kushika utakalo enn? Aaaa, nenda kwa Idi wako. Labda wewe usiwe damu yangu. Ila n’nakwambia: mwenda tezi na omo hurejea ngamani.”  

Kidawa naye alikwisha kata shauri. Akamkabidhi Mungu roho yake. Mungu na mtume wake na duniani kuna Idi. Hawezi kwenda kinyume na ahadi yake.

Ahadi ni deni. Hakutaka kuiwa kwa jambo analolimiliki na ambalo ana hiari nalo. Ingelikuwa fedha naye anajijua ni maskini, ingelikuwa nguvu zote alizonazo, ingelikuwa muhanga wa roho yake tamu … vyovyote vile angelikuwa tayari kuvitoa kwa ajili ya Idi. Seuze ile nafsi yake mwenyewe! Alikuwa tayari kumpa Idi yote bila ya kumsazia. Wala hapana aliyeweza kumzuia. Yu tayari kumfuata Idi hadi ukingoni mwa dunia, lakini hakuridhi kuolewa na dau hata kwa lulu zote duniani.

Toka siku hiyo Kidawa aliwachukia wazee wake kwelikweli. Alikichukia kila kilichokuwa chao. Alihisi kwa hivyo kuendelea kukaa nao ni kuzidi kula fadhila zao. Ina maana atakuwa anazidi kujitia katika masimango. Kusema kweli ni thawabu, Kidawa aliyachoka maisha ya kishamba; maisha ambayo hayakujali chochote juu ya furaha na maendeleo ya mwanamke wa kisasa; isipokuwa kupika na kupakua, kufua, kubeba mizigo ya kuni, kulima na kupalilia na kujitwika mahando ya maji. Basi wakae weeee, wazae kama panya, mpaka zao zifike. Na hayo ndiyo waliyomtakia wazee wake. Walitaka kumwua fo, huku anaona! Hawawahi! Yaliyompata sangara kutiwa moto yeye yamemkosa.

(Hadithi hii imetolewa kutoka Sadiki Ukipenda na Hadithi Nyingine, S.A. Mohamed, Jomo Kenyatta Foundation, Nairobi, 2002, kur.65-67).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *