Fasihi simulizi ni fasihi iliyo kongwe zaidi kwa sababu iliibuka pale binadamu alipounda lugha kama chombo cha mawasiliano. Ilikuwepo hata kabla ya uandishi kubuniwa. Hii ina maana kwamba hakuna jamii isiyokuwa na fasihi simulizi yake inayojikita katika lugha za jamii hiyo.
Sifa mojawapo ya fasihi simulizi ni kwamba ni ya kimapokeo, kizazi hukipokeza kingine fasihi hii hasa kupitia masimulizi. Ijapokuwa ina uhai na hubadilika kiwakati na kimahali, fasihi hii inategemea sana kumbukumbu ya msimulizi.
Jamii inapoibua kitu, hufanya hivyo ili kutimiza haja fulani. Kwa hivyo, fasihi simulizi nayo hutekeleza wajibu wake. Kutokana na ufinyazi wa kisanaa, fasihi hii hutekeleza jukumu la kustarehesha, kuburudisha na kuelimisha. Fasihi hii huburudisha kwa sababu nyingi. Kwanza, ni kutokana na lugha teule na usimulizi wa kuchangamsha uliojaa midundo ya sauti, vitendo na maigizo.
Fasihi simulizi huwa ina taswira, jazanda, mapambo, maigizo, taarifa halisi, na ushirikishaji wa hadhira. Hadhira inapoburudika na kufurahia sanaa kwa vicheko, vifijo na nderemo, huhisi vizuri nyoyoni na hupunguza mavune. Inasemekana kuwa kicheko ni dawa inayoshinda dawa zote. Hadhira inapocheka, hujiongezea afya kwa kufaidi chanzo cha kisanaa.
Tena fasihi simulizi huchangia sana katika kuendeleza na kudumisha historia ya jamii husika. Historia hii inaweza kudumishwa kupitia tanzu mbalimbali za fasihi simulizi. Kwa mfano, miviga – hadithi zinazohusu chimbuko la makabila – huweza kutufungulia mlango wa kuonea historia ya jamii. Fasihi simulizi, na historia ni vitu vyenye uhusiano wa kutegemeana.
Fasihi simulizi ni chombo cha kuelimishia jamii kuhusu asili yake, chanzo na
maendeleo ya utamaduni wake na maisha ya jamii hiyo kwa jumla. Kwa mfano, kupitia fasihi simulizi tunaweza kujua usuli wa utamaduni mseto wa Waswahii.
Tusomapo fasihi simulizi, fikra zetu hupanuka na tunapata fursa ya kujielewa vyema zaidi. Kujifahamu ni zana mwafaka ya kujiandaa kuikabili kesho. Lakini kujifahamu hakutokei mara moja bali hupitia hatua kadha. Hatua mojawapo ni kupokea vyombo vya sanaa vyenye vipopo vya fikra.
Inasemekana kuwa jamii isiyokuwa na maadili inaweza kujiangamiza. Njia mojawapo ya kuendeleza na kudumisha maadili ni kupitia fasihi simulizi. Utanzu wa ngano ni muhimu sana katika ukuzaji wa maadili. Ngano ni hadithi zinazotoa mifano ya maisha ya binadamu na matatizo yake. Dhamira kuu ya ngano nyingi ni kubainisha namna binadamu anavyoweza kuyamudu matatizo yake yaliyomkuza. Upeo wa maisha ya binadamu wa kuishi raha mustarehe baada ya mapambano makali hujitokeza na kumpa msikilizaji matumaini. Ngano huhimiza binadamu kufanya bidii maishani na kubadilisha maisha yake, kwani ‘Mvumilivu hula mbivu’ na ‘Mchumia juani hulia kivulini.’
Ukichunguza methali nyingi utaona kuwa zimejaa ushauri. Ushauri huu una manufaa kwa msikilizaji kwa sababu hutoa mwongozo wa maisha.
Wakati methali zikihimiza na kushauri, vitendawili ni vinoa bongo na vichemsha akili. Mtu anayepigiwa kitendawili huchemsha ubongo wake akitafuta jibu. Labda vitendawili humwandaa mtoto kufahamu hesabu.
Hurafa (hadithi zinazohusisha wanyama kwa wingi) licha ya kushauri, huonyesha uhusiano baina ya binadamu na mazingira yake. Wahusika wanyama hupewa sifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na lugha. Hapo binadamu hushauriwa kujifunza kutokana na ulimwengu wa wanyama.
Kwa upande mwingine, hekaya – zenye wahusika wajanja sana – ni mafunzo kuhusu ulimwengu na mikasa yake. Dhamira ya hekaya ni kuhimiza watu wasife moyo.
Ujumbe ni kwamba mtu akijikuta kwenye matatizo na mitego, afanye hima ajinasue na awanasue wengine. Hekaya za Sungura, ananse mtu-buibui au Abunuasi ni jazanda ya uhusiano baina ya udogo na ukubwa. Kulingana na hekaya hizo, ukubwa wa mwili si hoja; lakini ukubwa wa akili ndio ufunguo wa maisha.
Wahusika Mighani — hadithi zinazohusu mashujaa – ni himizo kuhusu ujasiri. wakuu wa mighani ni majagina na sifa yao kubwa ni usikawaida. Huwa wakubwa sana na wenye ujasiri mwingi. Lakini huwa wana unyonge fulani kwa sababu ni binadamu. Majagina huuawa kwa siri yao kufichuka! Ni kama kwamba msikilizaji wa mighani anaambiwa, “Hakuna kubwa duniani!”
Fasihi simulizi ina nafasi kubwa katika shughuli za binadamu na inatujuzu kuihifadhi na kuiendeleza. Kila mmoja wetu anaweza kuidumisha kutokana na utafiti na ubunifu. Tusiidhalilishe bali tuitukuze.