Fasihi simulizi ni sanaa ya lugha inayohifadhiwa kwa njia ya mapokezano. Ilitangulia fasihi andishi na inajishughulisha na maisha ya binadamu pamoja na mazingira yake. Kwa mfano, inaweza kuonyesha namna binadamu awezavyo kujiepusha na maangamizi kwa kujibunia mbinu bora za chakula, makazi na elimu. Inadhihirisha namna binadamu awezavyo kukabili mazingira tata ili ajinusuru.
Aina za fasihi simulizi
Kuna aina mbalimbali za fasihi simulizi: Tutafafanua chache.
(a) Ngano:
Hizi ni hadithi zinazoonyesha namna binadamu anavyoweza kutumia akili yake kuyamudu matatizo yaliyompata. Hadithi nyingi zinaonyesha kuwa juhudi, uvumilivu na maarifa huweza kuleta maisha bora na kumsaidia binadamu kufikia kilele cha matamanio yake. Huonyesha kuwa binadamu wavivu, walegevu, wanafiki, na dhalimu hawawezi kufaulu.
Wahusika wa ngano ni binadamu, wanyama, mazimwi, wadudu na kadhalika. Wahusika hawa hujengwa ili kuzungumzia maisha ya binadamu. Usimulizi katika ngano ni changamano na huchangia katika uelewekaji wa maudhui. Japo usimulizi ni wa mtiririko, hujumuisha pia nyimbo, mahojiano, maigizo, vichekesho, methali na majibizano kama mbinu za kisanaa na katika kujenga vyema maudhui. Ngano hutumia fani mbalimbali ili kuimarisha usanifu. Kwa mfano taswira, tanakali za sauti, taharuki, na chuku.
- Visasili: Hizi ni hadithi zinazojikita katika asili ya vitu au mambo. Visasili vinaweza kusimulia asili ya binadamu, dunia, magonjwa, kifo, na kadhalika.
- Hurafa: Hizi ni hadithi zinazotumia wanyama kwa wingi. Wahusika wanyama hupewa tabia za binadamu, pamoja na lugha. Hata hivyo, kinachozungumziwa ni maisha ya binadamu.
- Miviga: Hizi ni hadithi za imani. Kwa mfano, zinaweza kusimulia chanzo cha makabila. Maelezo ya miviga huwa hayana msingi wa kihistoria. Kwa mfano, kuna miviga ya Adamu na Hawaa, Gikuyu na Mumbi, na Mbodze na Matsozi.
- Hekaya: Hizi ni hadithi zinazojulikana zaidi kutokana na ujanja wa mhusika mkuu. Mhusika mkuu hujikuta katika mikasa mingi. Katika fasihi nyingi Sungura (anayeweza kulinganishwa na Abunuasi) anahusika katika hekaya nyingi. Dhamira ya hekaya ni kuhimiza watu wasife moyo bali wawe na moyo wa kujinasua.
- Mighani: Hizi ni hadithi zinazohusu ushujaa. Wahusika hawa huitwa majagina. Wapinzani wa majagina ni majahili, wasiojali kamwe maslahi ya watu wengine. Majagina wana sifa za usikawaida. Kwa mfano, uwezo wao si wa kibinadamu. Hata hivyo huwa wana unyonge mmoja, kwani ni binadamu tu. Kwa mfano, Uyahudini kuna mighani ya Samsoni na Delila na miongoni mwa Waluo kuna jagina Lwanda Magere.
(b) Misemo:
.
- Methali: Hili ni tamko linaloelezea wazo la busara kwa ufupi. Methali nyingi za Kiswahili zina takriri, vina, mizani, na tanakali za sauti. Methali zingine zina mizani kumi na sita, kama mshororo wa shairi. Ili kufahamu maana/matumizi ya methali ni muhimu kuzingatia lugha na mazingira.
Kwa sababu methali ni mkato wa hadithi ni vyema kujiuliza ujumbe ulioshehenezwa na methali husika. Methali zinaweza kuasa, kuhimiza, kukanya, kufahamisha, kuelekeza, kukashifu na kutanabahisha.
- Vitendawili: Vitendawili ni mafumbo ya maisha na ufumbuzi wake unaweza kutumiwa kuchanganulia na kuhakikia jamii. Vitendawili ni matokeo ya maana ya mazoea ya mazingira na kwa hivyo kadri mazingira yanavyobadilika ndivyo vitendawili vinavyobadilika. Vitendawili vinaweza kutumiwa ili kuchemsha bongo. Kwa mfano:
Tunda langu la ajabu: pia nyama, katikati ngozi, na ndani mchanga. Jibu: Firigisi.
Hapa kitendawili kinafundisha jinsi ya kufafanua sifa za firigisi kwa kuilinganisha na tunda. Anayetegewa sharti atumie mantiki. Pia humwezesha mtu kuweka kumbukumbu. Kwa sababu vitendawili hutegwa kwa mashindano, mtu hutakiwa afikiri upesi na atoe jibu.
Vitendawili vinafundisha kuhusu mazingira na vitu katika mazingira hayo. Ni himizo la mtu kuwa na uzingatifu.
Katika utanzu huu tunapata sitiari, tanakali za sauti na taswira.
Tazama:
Brururu mpaka Makka.
Jibu: Utelezi.
Nyumba yangu haina mlango.
Jibu: Yai.
(c) Nyimbo:
Hizi zinashughulikia maswala ya kijamii kama mapenzi, ndoa, kashfa, wasifu, vita, kifo, kuzaliwa na kadhalika. Nyimbo nyingi hutumia mbinu za kisanaa pamoja na mdundo wa kuimbika. Mashairi, kama tunavyoyajua siku hizi, yanatokana na nyimbo.