Nyimbo ni tungo zenye mahadhi. Mawimbi ya mahadhi au sauti hizo hupanda na kushuka kutegemea wimbo unaotongolewa. Kila jamii duniani ina nyimbo zake za kuelezea hali na hisia mbalimbali za maisha, mathalan; furaha/tafrija, tanzia, ushawishi wa kisiasa, sifa, kazi, na kadhalika. Baadhi ya nyimbo huambatana na ngoma au ala.
Wimbo ufuatao huimbwa na watoto wadogo.
HODI
Hodi, hodi ni nani Aliye hapo njiani?
Msafiri mwenye cheo
Na mzuri kabisa
Roho yangu ‘enda mbio
Nitamwitikia sa!
Sifa za nyimbo
Kwa kawaida, nyimbo huwa na sifa zifuatazo:
(i) Mapigo ya silabi.
(ii) Muundo wa lugha ya mkato.
(iii) Matumizi ya picha (au taswira).
(iv) Mdundo wa kimahadhi (kimuziki) au wizani.
(v) Msamiati mwepesi unaoeleweka kwa urahisi.
Umuhimu wa nyimbo katika jamii
(i) Nyimbo humpa msikilizaji na mwimbaji burudani nzuri.
(ii) Nyimbo hukosha, kukonga na kutakasa hisia za ndani zinazombana mwimbaji au msikilizaji. Baadhi ya hisia hizo ni kama vile huzuni, chuki, hasira, upweke na kutamauka. Nyimbo za nasaha hutekeleza jukumu hili.
(iii) Nyimbo huelimisha wanajamii kwa kuwapa maarifa mbalimbali.
(iv) Nyimbo hukuza na kudumisha utamaduni wa jamii mbalimbali,
(v) Pia, nyimbo hukuza na kuimarisha lugha kupitia matumizi ya msamiati, ishara na taswira.
(vi) Nyimbo huhifadhi kumbukumbu au rekodi za matukio muhimu ya Kisalua (kihistoria) katika jamii mbalimbali.
Nyimbo na ngoma za Waswahili
Jamii zote ulimwenguni zina nyimbo na ngoma zake. Ngoma hizi hutekeleza majukumu mbalimbali. Uainishaji wa nyimbo na ngoma hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
Aina Nyimbo
Nyimbo na ngoma za Waswahili zinaweza kuainishwa kama ifuatavyo:
- akika: nyimbo za kumtoa mtoto mchanga nje baada ya siku saba.
- bembea/bembezi: Nyimbo za kubembeleza watoto.
- tumbuizo: nyimbo za furaha au burudani.
- kimai: nyimbo zinazohusishwa na mabaharia na maisha ya wavuvi.
- wawe/vave: nyimbo za kufanya kazi; nyimbo za wakulima.
- nyiso: nyimbo zinazohusishwa na jando na unyago.
- nyimbo za dini.
- nyimbo za siasa.
- nyimbo za arusi.