Ufuatao ni mfano wa wimbo
wa taarab:
Nitakupa maarifa x4
Uketi ukiyaandika
Ashibaye hukinai x3
Hamjui mwenye njaa.
Nyimbo za taarabu
Nyimbo za taarab ni kielelezo bora cha ufanisi na uamilifu wa nyimbo miongoni mwa wanajamii wa mwambao wa Afrika Mashariki. ‘Taarab’ ni neno la Kiarabu lenye maana ya ‘furaha’. Ni muziki wa kustarehesha na kuwaburudisha watu wa matabaka yote. Hupoza machofu ya umma.
Aidha, ni aina moja ya fasihi simulizi inayotumika hasa katika sehemu za mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki. Ni maarufu sana Mombasa na Unguja Inasemekana kwamba taarab ililetwa Afrika Mashariki mnamo mwanzoni mwa 1870. Kuna madai kuwa Sultan wa Unguja Seyyid Barghash, aliyependa anasa na starehe, aliwaalika watribu kutoka Misri waje kumtumbuiza. Wenyeji wakavutiwa na muziki huu na wakajifunza kupiga vyombo na kuimba. Vyama vingi vya taarab vimeundwa tangu siku hizo kama vile Lucky Star, Black Star, na Muungano, na waimbaji maarufu kama vile Siti Binti Saad na Shakila kujitokeza.
Taarab hutumia lugha yenye mvuto. Aghalabu hutumia mtindo wa kishairi Ushairi utumikao zaidi ni ule wenye urari wa vina na mizani. Lugha ya kishairi husababisha matumizi ya lugha ya kiishara na mafumbo.
Kwa mfano:
Nakuonya tahadhari punguza kulirandia Sega langu la asali najua walinyatia
Utakufika muhali vya watu kuvivamia
Walinzi wake wakali mashujaa walotimia
Hata tembo mwenye hali hathubutu kusogea
Walinzi wake ambao wakali wasochelea
Bunduki na marisao wameshinda kufyatua
Mikuki na zao ngao ni bure wamekimbia
Seuze we mwanakwao huna unachokililia
Umepigwa mpumbao mate unakimezea
Wameshindwa wenye vyao seuze wewe raia?
Kiitikio:
Hebu acha kujigamba huna unachokipata
Haiwi tembo na simba umewashinda ukuta.
Taarab, japo ni muziki wa starehe, si ngoma ya starehe tu. Inafanya kazi ya kuwaraghibisha wananchi kiitikadi. Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere nchini Tanzania, kwa mfano, taarab ilitumiwa kuendeleza siasa ya Ujamaa. Ushairi huu hutoa mawaidha mema kwa wanajamii. Tazama taarab ifuatayo kuhusu ujana.
Ujana umenipoteya, kama moshi siuoni
Na nguvu zimenitoka, hazimo tena mwilini
Na sasa nimeshakuwa, nimeingia uzeeni
Shujaa nilikuwa ya kweli namwambieni
Na nguvu zilinijaa sikuhofu asilani
Na sasa nimeshikwa, sina raha duniani
Dunia ina hadaa hilo nimeliamini
Dunia ina fazaa sasa nimekuwa duni
Sasa nimeshachakaa, na ujana siuoni
Majuto yamenijaa sijui nifanye nini
Kwa mambo yalotokea, mimi kwenda uzeeni
Wala sikufikiria, hayakuja akilini
Kiitikio:
Uwapi ujana wangu, ule nikijivunia
Umepita kama moshi, mara umeshapotea.
ZOEZI
(a) Taarab ilizinduliwa vipi katika maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki? (
b) Muziki wa taarab unatumiwa kwa shughuli gani za kijamii?
(c) Eleza maana ya:
(i) uamilifu