Insha ni mtungo wa maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya nathari au mchezo wa kuigiza (drama). Maneno yenyewe hupangwa kimantiki katika sentensi; mfululizo wa sentensi zinazohusiana na mada inayoshughulikiwa hupigwa mafungu ya aya (katika nathari) au uzungumzi (katika mchezo).
Kwa vile insha ni kazi ya sanaa na ya kubuni, lugha inayotumiwa ni yenye mvuto, iliyosheheneza semi, methali na tamathali nyingine za usemi.
Aina za insha
Tuna aina mbalimbali za insha kama ifuatavyo:
Masimulizi: Hujishughulisha na kusimulia kisa au visa kwa kutumia maelezo ya mfululizo.
Mjadala: Huzua, kutetea na kupinga aina fulani ya mawazo kwa misingi ya uthibitisho ulio dhahiri.
Kubuni: Hutumia msingi fulani wa uhalisia (ukweli) katika kujenga hadithi ambayo kwa kweli haikutokea. Mtunzi mzuri wa insha hubuni visa au matukio yanayoweza kuaminika kwa urahisi.
Wasifu: Hueleza sifa za watu, vitu au mahali. Insha za wasifu zaweza kuwa halisi au za kubuni, yaani mwandishi anaweza kusifu mtu, kitu au mahali anapojua au alipobuni.
Maelezo: Hutoa maelezo mfululizo kuhusu tukio au jambo, jinsi mwandishi anavyofahamu.
Mazungumzo/ Dayalojia: Huhusu mazungumzo ya ana kwa ana baina ya watu au makundi mawili. Mahojiano pia yanakurubiana kimtindo na mazungumzo.
Hotuba: Ni uzungumzi wa mtu huku hadhira yake inamsikiza. Hadhira haitarajiwi kumkatiza mzungumzaji kwa kumwuliza maswali papo hapo.
Barua: Ni wasilisho la maandishi la kirafiki au kirasmi. Barua huwa na kaida za kimapokeo zinazokubalika kimataifa.
Picha: Ni habari zinazowasilishwa kimchoro. Mwandishi hutarajiwa kugeuza mchoro kuwa maandishi kwa mujibu wa ruwaza anayoipata kutokana na michoro hiyo.
Methali: Ni mtungo unaotokana na ada, maana au mafunzo ya methali fulani mahsusi.
Kumbukumbu: Ni rekodi au hifadhi ya utaratibu wa mkutano inayoratibiwa na kuandikwa na katibu.